anzania imejaaliwa kuwa na kampuni na taasisi kadhaa zinazohusika na mawasiliano na nyingi ni binafsi zinazojiendesha kwa faida kubwa kabisa haswa za mawasiliano ya simu na mitandao yaani internet .
Kampuni hizi na taasisi zote zinafuata miongozo kutoka tume ya mawasiliano Tanzania yaani TCRA ambayo ndio mdau mkuu wa mawasiliano nchini kwa kushirikiana na idara nyingine ndani ya serikali ,kimataifa kama umoja wa mataifa na taasisi nyingine za jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama .
Kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita mpaka sasa kumekuwa na migogoro ya hapa na pale inayohusisha TCRA , kampuni za mawasiliano haswa Simu na Internet ,Watumiaji wa Huduma hizi na Taasisi nyingine haswa zinazohusiana na Afya , Mazingira na Miundombinu .
Migogoro yenyewe ni kama Ifuatavyo .
1 – Mfumo wa Kodi wa huduma za mawasiliano haswa simu na Internet ( mara kadhaa imepigwa kelele kwamba na wadau ) kwamba kampuni hizi zinakwepa baadhi ya kodi au kulipa pungufu huku serikali haina taarifa za kutosha kuhusu uendeshaji wa kampuni hizi .
2 – Umiliki wa Minara ya Mawasiliano umekuwa tatizo sugu ,kwa mfano kampuni za simu huwa zinalipa wenye kiwanja au nyumba hela Fulani kwa ajili ya kuweka mnara sehemu hiyo , mnara ambao unahudumia maelfu huku wilaya , mtaa au mkoa haufaidiki vya kutosha na uwekezaji huo .
Kwa siku za karibuni zimetokea kampuni kama ETON towers zinazonunua minara na kutaka kuimiliki , hilo hata hapa Tanzania limeanza kufanyika na haijulikani Serikali inahisa kiasi gani kwenye Kampuni hizi na ulinzi na usalama wa mawasiliano yetu ukoje .
Kuna sehemu unaweza kukuta minara zaidi ya 4 ya kampuni 4 tofauti yote imegharibu fedha nyingi , hapo uharibifu wa mazingira unatokea ,afya za majirani zinakuwa mashakani wanaoathirika ni watanzania wenzetu .
3 – Kampuni za Simu Kuuza Hisa
Kumekuwa na malalamiko toka kwa watanzania kuhusu kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni hizi kwa kununua hisa kama ilivyofanya safaricom nchini Kenya kwa kuuza hisa zake kwa wananchi wa nchi hiyo , jambo hili limekuwa likipigwa dana dana na kuonekana kama vile haiwezekani na watu kutoa sababu kadhaa kwa mfano kampuni zaweza kushusha gharama za mawasiliano na mengine yanayohusiana na hayo .
La msingi ni kujua kwamba kampuni za mawasiliano ya simu kwa sasa zinafanya biashara mbalimbali sio upigaji wa simu tu , kuna huduma za internet kutumia simu za mikono au vifaa vinavyochomekwa kwenye kompyuta , wanatoa huduma za kuhifadhi na kutuma fedha ( kama mpesa , ezypesa na Tigo pesa ) kwanini wananchi wasiwe sehemu ya umiliki wa huduma nyingine zinazotolewa na kampuni hizi ? Tafakari .
4 – Sheria za Mawasiliano
Hapa nchini tuna sheria moja ya mawasiliano ya Elekroniki na posta kwa jina la EPOCA , sheria hii haijatazama masuala ya fedha , taarifa binafsi za watu , na huduma nyingine zinazotolewa na kampuni za mawasiliano haswa zinazohusu mitandao ya kijamii na barua pepe .
Ni vizuri sheria hii iangaliwe upya ili iendane na wakati wa sasa na ujao kulingana na ushindani wa kibiashara ulipo na kuangalia maslahi ya watumiaji wa vyombo vya mawasiliano .
Kama nchi imeshindwa kuunda sheria zake za mawasiliano bora kutumia zile za jumuiya mbalimbali kama za umoja wa ulaya , jumuiya ya madola .
Kuna kesi nyingi zinazoendelea za uhalifu wa kimtandao ambazo zinahitaji uwepo wa sheria kali na miongozo kwa ajili ya uendeshaji wake na hukumu .
Mwisho .
Kwa kuandika haya napenda kuomba wadau mbalimbali haswa wabunge kuandaa hoja binafsi ya kuhakikisha masuala haya yanajadilika na wananchi waweze kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni hizi na wawe na sauti juu ya uendeshaji wa kampuni hizi kupitia hisa zao na vyombo vingine vilivyopo kisheria .
Pia kuundwe chombo kingine binafsi kinachoweza kusimamia njia za mawasiliano na miundombinu yake , pale kampuni inapotaka kuweka mnara sehemu au kuweka miundombinu Fulani basi kampuni hii ndio ihusike na ilipwe na ndio iwe msimamizi wa sekta hii muhimu inayozidi kukuwa kila siku .
Kwa kufanya hivyo tutatengeneza ajira nyingi , kuipunguzia mzingo TCRA , miuondombinu itaweza kulindwa kwa uhakika na hata kuweza kushugulikia baadhi ya vitu kwa haraka zaidi .
Tuunde chombo huru .
Na:Yona Maro