Friday, October 26, 2012
UGANDA YAPANIA KUDHIBITI MITANDAO JAMII
Moja ya sehemu iliyofanikiwa kufanya mapinduzi makubwa ya teknolojia ya sayansi ni teknolojia ya habari na mawasiliano.
Katika mapinduzi hayo ya teknolojia ya mawasiliano kumeibuka mitandao mingi ya kijamii ikiwamo Yahoo,Gmail,Twitter,Facebook,Youtube,blogs na mingine mingi ya aina hiyo.
Kama ilivyo kwa mapinduzi mengine yanayotokea huwa na faida na hasara.Kwa hapa Afrika mitandao hiyo imeonekana kuwa mwiba kwa serikali nyingi ambako katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikitumiwa kuhamasisha wananchi na kufanya maandamano ambayo husababisha kung'oa tawala mbalimbali ikiwemo Libya,Misri na Tunisia.
Hivi karibuni nchini Uganda wamejikuta wakikumbwa na hasara za mitandao hiyo baada ya kutumia na kiongozi wa upinzani,Kiiza Besigye kuhamasisha maandamano ya kuing'oa serikali.
Kwa Uganda ilishindikana kutokana na wananchi wengi wa nchi hiyo kushindwa kupata ujumbe huo kutokana na wengi wao kutokuwa na mitandao au wengi wao kutokuwa na fedha za kutosha za kuingia katika 'internet cafe' .
Kutokana na tukio hilo Polisi nchini Uganda wametangaza nia yao ya kudhibiti matumizi zaidi ya mitandao jamii kutokana na hofu ya kusambaa kwa habari zinazozua tishio kwa usalama wa nchi
Hayo anayasema Ofisa Mkuu wa Polisi wa Uganda Jenerali Kale Kayihura kwenye mkutano wa wakuu wa polisi kutoka kanda ya Afrika Mashariki
Taarifa hii ya polisi inakuwa wakati wafuasi wa upinzani wakiwa wametumia mitandao ya kijamii kuwasiliana.
Kayihura katika hotuba yake kwa wakuu wa polisi kutoka Afrika Mashariki pamoja na wajumbe toka Tanzania,Sudan,Sudan Kusini,Somalia,Sychelles,Burundi,Kenya,Rwanda,Ethiopia,Eritrea na Djibuti alisema mitandao ya kijamii ni mizuri lakini inaweza kuwa mbaya kwa jamii kwa sababu inatuma ujumbe haraka.
Mwaka 2009 watu 21 walifariki katika ghasia mjini Kayunga,Uganda kufuatia taarifa kuhusu ziara tata ya mfalme mmoja wa kitamaduni.
Inaelezwa kuwa hivi karibuni vijana nchini Uganda wameanza kutumia mitandao hiyo kujadili mambo ya siasa,wakifananisha matumizi ya mitandao hiyo kuleta mageuzi kama inavyofanyika katika nchi za kiarabu ambapo mtandao wa facebook ulitumika kuhamasisha watu na kuwaleta pamoja kwa sababu za kisiasa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima