Thursday, December 31, 2015

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA BARUA PEPE ZA KAWAIDA KATIKA MAWASILIANO YAKE



Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. 
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (katikati) akiwasili Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao kwa ziara ya kikazi leo jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. 
Mkurugenzi wa Uratibu wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao Bw. Benjamin Dotto akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini leo jijini Dar es salaam. 



Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akizungumza na Watendaji na baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala ya Serikali Mtandao leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam. 
 
Serikali imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao. 

  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini. 

  Ameeleza kuwa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi ambayo ni ndogo lazima iongezeke, hivyo serikali haiwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huo huku akifafanua kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi. 

Amesema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEKINOHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEKINOHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali. 

Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano huku akitoa siku 60 kukamilika kwa zoezi hilo katika taasisi zingine.


Popular Posts

Labels