Kasisi mmoja nchini Italia, ameweka kifaa kanisani mwake
kinachoweza kubana mawasiliano ya simu baada ya kuchoka kuwaomba waumini kuzima
simu zao kila wakati alipokuwa anahubiri.
Alilazimika kuomba idhini ya polisi kuweka kifaa hicho baada
ya kuchoka kusikia milio ya simu zikipokea ujumbe.
Mpango huo umesifiwa sana na waumini ingawa imewaudhi wenye
maduka katika mji wa Naples wanaosema kifaa hicho kinatatiza masafa na
mawasiliano yao na pia kifaa hicho kimeathiri mashine za kutoa pesa.
Wanasema kifaa hicho pia kinatatiza shughuli zao ambapo
wateja huagiza bidhaa kupitia simu zao za mkononi.
Kasisi Don alikasirishwa sana na waumini wake kujibu simu
zao wakiwa kanisani
Lakini kasisi Don Michele Madonna, anakana kwamba kifaa
chake kinatatiza shughuli za wenye maduka akisema kinaathiri tu mawasiliano kwa
simu kwa waumini walio kanisani peke yake.
'Nilinunua kifaa hicho kutoka kwa duka la vifaa vya
elektroniki, na kuwauliza polisi ikiwa ilikuwa sawa kuweka kifaa hiicho
kanisani mwangu. Ni kifaa kizuri sana kwa sababu kimemaliza tatizo la watu
kupigiwa simu na kuzipokea wakiwa kanisani.
Mmiliki mmoja wa maduka alisema: 'Tangu kasisi Madonna
kuweka kifaa hicho ndani ya kanisa , nimepata matatizo sana kutumia kadi yangu
katika biashara yangu. ''
Kasisi Michele Madonna aliamua kuchukua msimamo huo kwa
sababu waumini walikuwa na mazoea ya kutumia simu zao kanisani wakati kasisi
huyo akihubiri. Kilichomuudhi zaidi kasisi huyo ni watu kupokea simu kanisani
na hata wakati wa mazishi.
Kasisi Don alinunua kifaa hicho kwa dola sitini.
Kabla ya kukinunua kifaa hicho alianza kwa kuwasihi waumini
kutotumia simu zao kanisani kwa sababu zilitatiza shughuli zake.
Alianza kwa
kuweka mabango kanisani humo lakini ujumbe huo wengi hawakuuzingatia na hapo
ndipo akalazimika kuweka kifaa hicho ambacho kinazuia watu kupokea au hata
kutumia simu zao kanisani.