Bwana. Keriako Tobiko |
Mkurugenzi
wa Mashtaka ya umma ya nchini Kenya Bwana. Keriako Tobiko ametangaza kuanzishwa
kwa kitengo maalumu kitakacho pambana na
uhalifu mtandao katika ofisi yake. Amedai hatua hii imefikiwa kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya uhalifu unaofanywa na wahalifu wenye uelewa wa
teknolojia.
"Kwa
mtazamo wa kuongezeka kwa uhalifu wa mtandao, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
wa Umma (ODPP) imeanzisha kitengo maalumu kusimamia mashtaka ya wahalifu wa
mtandao," Tobiko alisema, kwa mujibu wa The Standard la Kenya.
Takwimu
zinaonyesha Kenya inapoteza kiasi cha shilingi bilioni 2 (Dola milioni 23.3)
kwa mwaka kupitia uhalifu wa mtandao." Aliongeza Bwana Tobiko.
Hata
hivyo, alisema, jitihada za kuwakamata na kuwashitaki watuhumiwa zimekua ngumu
kutokana na ukosefu wa sheria zinazofaa, zikiwaacha huru wahalifu kufanya
uhalifu wa mtandao ambao unatishia usalama wa taifa, miundombinu ya teknolojia
ya habari na mawasiliano pamoja na haki ya usiri wa raia.
"Kwa
kutambua kwamba kwa sasa kuna sheria zisizotosheleza za kushtaki uhalifu wa
mtandao, ODPP imeandaa warsha ya kupitia upya sheria zilizopo na kuandaa rasimu
ya mswada wa kina kuhusu uhalifu wa mtandao kulingana na taratibu husika za
kimataifa zinazofaa," Tobiko alisema, akiongeza kwamba matumaini ya kuwa
na mswada wa kina wa uhalifu wa mtandao yatakamilika mwaka huu.