Maafisa wa utawala katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamebana matumizi ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi baada ya kusema kuwa ni tisho kwa usalama wa nchi.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano serikali.
'Wenye simu za mkononi hawaruhusiwi kutuma ujumbe mfupi kuanzia Jumatatu 2 Juni 2014 hadi itakapotolewa taarifa zaidi kuhusu agizo hili,'' huu ndio ulikuwa ujumbe wa wizara ya mawasiliano kwa kampuni za kutoa huduma za simu.
Inaarifiwa kuwa uamuzi huo ulifikiwa na waziri mkuu Andre Nzapayeke.
Tangu wiki iliyopita, kumekuwa na ghasia zaidi mjini Bangui, pamoja na kutolewa wito wa maandamano uliotumwa kwa simu kama ujumbe mfupi siku chache zilizopita.
Duru zinasema kuwa hatua ya kubana ujumbe mfupi wa simu itadumu kwa siku kadhaa kabla ya agizo lengine kubatilisha amri hiyo.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inakumbwa na vita kati ya jamii za wakristo na waisilamu imekuwa ikikumbwa na hali ngumu ya usalama pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya jamii hizo
Chanzo:BBC