Saturday, June 7, 2014

TUJIFUNZE KUTOKANA NA CHINA KUKATAZA WINDOWS 8

Katika wiki chache zilizopita kulikuwa na msuguano kati ya serikali ya Marekani na China , Serikali ya Marekani inailaumu china kwa kufanya udukuzi kwenye kampuni zake na biashara nyingine huku china nayo ikiilaumu marekani na mwishowe ikaamua kukataza matumizi ya windows 8 kwenye kompyuta zote za serikali na taasisi zote zinazopewa fedha na serikali ya nchi hiyo .

Serikali ya China na wataalamu wake kadhaa wanasema matumizi ya windows 8 ni hatari kwa usalama wao na ustawi wao , kwahiyo wamekataza na kuendelea kutengeneza program yao ya COS China Operating System kwa ajili ya matumizi ya serikali pamoja na taasisi zake .

Kwan nchi za ulaya suala kama hili liliwahi kutokea miaka kadhaa iliyopita , lakini umoja wa ulaya ulienda mahakamani na mahakama ikaamua Microsoft itoe source code kwa umoja wa ulaya ili waweze kubadilisha na kuweka mambo yao kwa maslahi ya umoja wa ulaya .

Kitu kikubwa ambacho serikali ya uchina inalalamikia kuhusu Windows 8 ni hii source code , serikali ya china inataka source code ya bidhaa hii ili iweze kuifanyia mabadiliko iendane na maslahi yake haswa kwenye mambo ya ulinzi na usalama .

Hapa nchini kwetu tumeona taasisi mbalimbali na wizara mbalimbali za serikali tena nyeti zikitumia bidhaa mbalimbali za windows bila kufanya mabadiliko yoyote kwa ajili ya usalama wao , tumeona watu haswa viongozi wakinunua kompyuta na vifaa vingine vya mawasilino na kuvitumia kuhifadhi taarifa nyeti bila vifaa hivi kuchunguzwa au kubadilishwa chochote .

Suala la serikali ya China lituamshe na tuanze harakati za kuangalia maslahi makubwa ya taifa wakati wa manunuzi na matumizi ya vifaa na program mbalimbali toka nchi za nje , program hizi na vifaa vyake vinaweza kutumika kwa urahisi kuhamisha taarifa na chochote kile au kufanya uhalifu bila mnunuzi au mtumiaji kujua .

Wakati serikali inafikiria kupeleka muswada wa sheria ya usalama wa mtandao bungeni , ni vizuri suala kama hili lijulikana na wataalamu watakaojadili sera au chochote kinachohusiana na usalama wa Taifa .

Huwezi kulinda taifa kama taarifa zako zinaweza kuchukuliwa au kuangaliwa na mtu akiwa popote duniani .

YONA F MARO 
0786 806028

Popular Posts

Labels