Meneja Masoko na Usambazaji Huduma za Kifedha wa Tigo, Catherine Rutenge (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Kampuni inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali Tigo imetangaza gawio jingine la robo mwaka la shilingi bilioni 6.04 (sawa na dola za Marekani 2,763,636) kwa watumiaji wa Tigo Pesa ikiwa ni mara ya kumi katika mfululizo wa kampuni hiyo ya simu kugawa faida hiyo kwa watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa njia ya simu.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo Ruan Swanepoel alisema kwa ujumla kampuni hiyo imeshawalipa watumiaji wake wa huduma za fedha kwa njia ya simu jumla ya shilingi bilioni 52.28 (sawa na dola za Marekani 23,763,636) ikiwa ni malipo ya robo mwaka ya kumi tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo Julai 2014.
Hii ni mara ya tatu kwa mwaka huu kwa Tigo kulipa gawio kwa wateja wake.
Swanepoel alisema kuwa katika robo ya tatu ya mwaka huu kiwango cha faida kilipanda na kufikia asilimia 9 ikiwa kimepanda kwa asilimia 1 kutoka robo ya pili ambako kumechangiwa kwa kiwango kikubwa na kiwango kizuri cha riba katika mifuko ya dhamana ndani ya benki mbalimbali za biashara.
Aidha alidokeza kuwa ongezeko kubwa katika kiwango cha gawio kumechangiwa na kuongezeka kwa faida, kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kukua kuliko imara kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama nyenzo kuu katika ongezeko kubwa la kiwango cha faida hususani katika kundi la wafanya biashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa wafanya biashara zaidi ya 50,000.
Mwaka 2014 Tigo Tanzania ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani kugawa faida iliyozalishwa na fedha za simu zilizopo katika Akaunti ya Udhamini kwa kipindi cha robo mwaka kwa wateja wake.