Shule ya Msingi ya Mlimani iliyopo Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kuanzia wiki hii itaanza kunufaika na huduma ya intaneti
bure inayofungwa shuleni hapo na Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wahabari Jijini Dar
es salaam Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Upendo Kujerwa ameshukuru msaada huo na
kusema kuwa ni muhimu na utawawezesha wanafunzi katika shule yake kuingia
katikaulimwengu wa sayansi na teknolojia ya kompyuta.
Kujerwa amesema, sasa wataweza kumudu vizuri
kusoma kwa kutumia kompyuta kwani sasa wataweza kupata elimu kwa nadharia na
vitendo ikiwemo kupata maarifa kutoka kwenye mtandao wa intanenti.
Aidha amesema pamoja na athari za matumizi
mabaya ya teknolojia, lakini ina mengi mazuri hivyo watahakikisha wanatumia
msaada huu kuwapatia maarifa mazuri wanafunzi wao maarifa ambayo yatawafaa
katika siku za usoni kwa kuwa miongoni mwa wataalamu wanaohitajika kwenye fani
mbalimbali ilikuendeleza taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake,
mwanafunzi Rose Mfinanga ameshukuru kwa msaada huo na kusema utawasaidia kujua
somo la kompyuta na kupata maarifa kupitia mtandao wa intaneti.