Friday, August 14, 2015

USALAMA MITANDAO: TANZANIA INA CHA KUJIFUNZA KUTOKA KENYA.

 
Nimekamilisha vikao vya usalama mitandao vilivyofanyikia jijini Nairobi kufuatia mualiko maalum nilioupata. Katika vikao hivyo niliwasilisha mada mbili (ya kwanza ikiwa ni namna ya kukabiliana na uhalifu mtandao na mada ya pili ikiwa ni namna ya uchunguzi wa makosa ya digitali kitaalam) katika mada hizo mbili ambazo zilipokelewa vizuri na kupelekea mijadala ya kipekee kuna mengi  nikajifunza kutoka kwa washiriki. Aidha, nilishiriki mijadala duara iliyojikita katika changamototo mbali mbali za uhalifu mitandao na kuiangazia sharia mtandao ya nchi ya Kenya.

Kenya ni miongoni mwa nchi tatu barani afrika ambazo zimeorodheshwa kuwa na uhalifu mkubwa sana wa kimtandao nyingine ni Nigeria pamoja na Afrika ya Kusini. Tukijadili takwimu za kutisha duniani kote, tulishuka na kuangazia bara la Afrika na baadaye Afrika Mashariki na hatimae kujikita na twakwimu za nchi ya Kenya.

Kwa upande wa Kenya kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika mkutano, hadi kufikia Mwezi wa saba mwaka huu (2015) kuna simu 34.8 Milioni  huku watumiaji wakiwa ni 26.0 Milioni. Aidha, matumizi ya intaneti ni 29.1 milioni ambayo ni sawa na 65% “penetration”. Takwimu hizo zinasindikizwa na upotevu wa dola za kimarekani 20 milioni ($20 Mil) kila mwaka kutokana na uhalifu mtandao.

Palizungumzwa matukio ya kudukuliwa kwa tovuti nchini humo ambapo, tovuti za serikali 103 ziliathiriwa mwaka 2013, na 3 kwa mwaka wa 2014 huku twitter ya serikali mwaka jana (2014) ikiwa ni miongoni mwa zilizo dukuliwa na kutumiwa vibaya. Nilihoji tofauti kubwa ya udukuzi wa tovuti na kujulishwa baada ya tukio la aina yake la mwaka 2013 serikali iliamua kuzifunga tuvuti zake nyingi hasa zile zilizo onekana hazina umuhimu sana kua hewani kitu ambacho kilichangia kupunguza namba kubwa ya udukuzi kwa mwaka 2014.

Kwa upande wa pesa zinazopotea kwa nyia ya simu – Miamala inayofanywa kwa njia ya simu ni asilimia kumi (10%) ya fedha za miamala yote kila mwezi huku idadi hiyo kuonekana kushtusha wengi.

Ikumbukwe nchi ya Kenya, matumizi mabaya ya mitandao yalisababisha kuchochea na kutokea vurugu zilizosababisha matatizo makubwa sana kipindi cha uchaguzi kilichopita ambapo kwa mujibu wa mchambuzi mmoja wa maswala ya uchanguzi alichapisha andiko na kueleza mitandao ilikua chanzo kikubwa cha kueneza chuki na fujo kipindi cha uchaguzi uliopita.


Yote hayo – Takwimu zote hizi kwa nchi ya Kenya zimesababishwa na jambo moja zuri sana ambapo ni kua na uwazi wa takwimu na taarifa za kihalifu mtandao ambapo kwa Afrika imekua ni nchi pekee iliyofanikisha swala hili. Itakumbukwa nilitoa pongezi kwa nchi hiyo baada ya ku ainisha takwimu zake kwa mara ya kwanza mwaka jana (2014) na kufanya iwe ya kwanza Afrika katika hili.

Kilicho nifurahisha zaidi ni hatua taifa hilo limechukua kukabiliana na uhalifu mtandao. Tayari nchi hiyo ina “National cybersecurity master plan” na sheria mtandao ambapo kosa la udukuzi adhabu ni miaka kumi (10) jela, faini ya KSH 10,000 au vyote kwa pamoja. Pia ina strategy ya maswala ya usalama mitandao na kupitia mamlaka ya TEHAMA “ICT Commission” wamesha zindua andiko linalotoa muongozo wa kuwalinda watoto katika mitandao.

Hayo ni uchache katika mengi ambayo tayari taifa limeweka katika mikakati yake. Zaidi ni mikakati ya kukuza uelewa na ujuzi kwa watu wake ili kuweza kuendelea kutumia vizuri mitandao pamoja na namna ya kukabiliana na uhalifu mtandao.Aidha, Mpango wa serikali kuimarisha ushirikiano ambapo CERT – KENYA inajumuisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama huku mashirika binafsi yakiwa na nafasi kubwa kuisaidia ili kukabiliana na uhalifu mtandao. Mfano wa Hili ni mshiriki kutoka Microsoft alipo tolea ufafanuzi kampuni hiyo inavyo fanya kazi karibu na serikali ya kenya kukabiliana na uhalifu mtandao nchini humo kupitia CERT –KENYA.

Kilicho nipa faraja kubwa ni kauli ya pamoja kua Kenya imefanya mengi lakini pakakubalika kua kuna mengi bado yakufanyia kazi ili kuweza kupiga hatua zaidi katika maswala ya usalama mitandao nchini humo. Ni marachache sana mataifa yanakiri kua bado safari ni ndefu ili kufikia malengo. Pamoja na hatua kubwa nilizo ziona katika nchi hiyo lakini bado walikiri kuna safari ya kupiga ili kusonga mbele zaidi.

Tulipata kuangazia aina za uhalifu na namna zinavyofanyika kwa nchi ya kenya – hakika aina hizi hapa kwetu pia ziko njiani na hofu yangu kubwa ni kwa kiasi gani tutakua tumejiandaa? Kujua tatizo nihatua za awali za utatuzi na wengine wakinyolewa ni vizuri tukatia nywele maji.

Kwa ufupi mambo yakufanyiwa kazi ambayo bado ni changamoto kwa mataifa yote yaliyoweza kujadiliwa ni pamoja na:-

Bado kumekua na dhana kua swala la usalama mitandao ni la kundi fulani ( wana TEHAMA – waliojikita katika maswla ya usalama mitandao) Hili sasa linatakiwa libadilike na katika kila kampuni au serikali lazima swala hili lianzie katika ngazi ya juu kushuka hadi ngazi ya mmoja mmoja (Kila mtu)

Bado udukuzi na uhalifu mtandao kwa ujumla umeendelea kushika kasi huku ugunduzi wa tukio kutokea kuchukua hadi siku 200 kwa wastani baada ya tukio ambapo tumekubaliana kimsingi hii ni namba kubwa sana na kunakila sababu ya kushusha namba hizi – pia kuwe na njia za kuzuia tatizo kabla halijatokea ambazo ni madhubuti kwa kufanyia kazi ushauri unaotolewa wataalam.

Uhalifu wa ndani (Insider threats) bado ni changamoto kubwa sana katika anga ya dunia na imeonekana kusahauliwa kabisa huku jitihada za dhati zikianza kuonekana kukuza uelewa kwenye hili na sasa tayari “Mr. Robot” tamthilia mpya ya kukuza uelewa wa maswala ya usalama mitandao imejikita kwenye hili.

Uhaba wa wataalam katika maswala ya usalama mitandao ni la kuchukuliwa hatua za haraka kwa kuhimiza mitaala ya usalama mitandao kuingizwa vyuoni huku wataalam wanaopatikana kutumika vizuri – Wenye ujuzi watumike mahali husika kwani imeonekana bado kuna changaoto ya kutotumiwa vizuri wataalm wa maswala haya inaypelekea uhalikfu kukua kwa kasi kila kukicha. Hili limeonekana zaidi barani Afrika na mataifa kadhaa wamesha anza kulifanyia kazi ili kuweka mabo sawa.

Sheria mitandao kutumiwa ipasavyo lakini pia iambatane na kua na waelewa wa uchunguzi wa makosa haya kwa kuzingatia maadili na taratibu za kitaalm zilizo sahihi na kuhakiki uelewa unasambazwa kwa watu ili kuepusha wimbi kubwa la wahalifu mtandao wanao fanya uhalifu huu bila kujua kuingia matatani – Imeonekana bado kuna ugumu mkubwa wa kesi za uhalifu mtandao kuvuka mahakamani na watuhumiwa kuwajibishwa kutokana na udhaifu mkubwa kwa mataifa ya Afrika mashariki walionao katika kufata taratibu za kuwasilisha kesi hizi ipasavyo mahakamani (Ujuzi bado Uko chini sana).

Ushirikiano wa ndani ya mataifa pamoja na kuvuka mipaka bado ni changamoto inayo onekana kuzikumba Nchi nyingi hasa barani Afrika huku Kenya ikiwa imeliona hili na imepiga hatua nzuri kwa ndani ila bado wanakiri kuvuka mipaka bado ni changamoto kutokana na utayari wa mataifa mengine katika hili.

Hayo ni kwauchache tu kwani mengi sana yamejadiliwa na nategemea kutumia muda wangu kadhaa kuwasilisha kidogo kidogo ili tuweze kuendelea kujifunza zaidi kupitia vyanzo mbali mbali vya habari.
NA:Yusuph Kileo

Popular Posts

Labels