Wananchi wanaotumia vibaya mitandao huenda wakajikuta matatani hivi karibu kwani Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuwa ifikapo
Septemba mosi, mwaka huu, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao itaanza kutumika humo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Meneja Mawasiliano wa TCRA,
Innocent Mungy amekiri kuwa pamoja na kwamba mamlaka hiyo imefanya kazi kubwa
ya kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi yake
si mazuri hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kwa sasa Tanzania
inaongoza kwa kuwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, jambo
linalosababisha taarifa za mitandao mingi kutoaminika hadi nchi za nje kutokana
na kujaa uzushi, uongo, lugha za uchochezi na picha za matusi.
Amesema kutokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya mitandao
nchini, kwa sasa nchi nyingi haziamini tena taarifa za mitandao ya kijamii na
wala hawazitumii hali inayopaswa kubadilishwa.
Mungy amesema mamlaka hiyo kazi yake kubwa ni kusimamia
matumizi ya mitandao hivyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola,
itahakikisha inadhibiti kwa kuelimisha na kuwabaini wale wote wanaotumia vibaya
mitandao hiyo.