Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yussuf Mwenda akibofya kompyuta kuzindua huduma ya WiFi ya bure kwenye Kituo cha Mabasi cha Sinza, wilayani humo, Ijumaa, Desemba 12, 2014 |
Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar
es Salaam, imedhihirisha jitihada zake za kwenda na wakati katika masuala ya teknohama, baada ya kuamua kutoa huduma ya bure ya mtandao wa intaneti wa
WiFi kwenye Kituo kipya cha Mabasi cha Sinza, jijini Dar es Salaam.
Akizindua huduma hiyo Desemba 12, Meya
wa Manispaa ya Kinondoni, Yussuf Mwenda amesema, mtandao wa WiFi
umeunganishwa kwenye kituo hicho kupitia mkongo wa mawasiliano kupitia
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Mwenda amesema, mtandao huo
utakuwepo usiku na mchana na kila mwenye kompyuta au simu zenye uwezo wa
kunasa Wi-Fi ataona katika simu au kompyuta yake akitaarifiwa kuwepo
mtandao wa bure wa KMC_FREE WiFi.
Alisema, mdau atakachofanya ni
kujinga bure na kuendelea kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za tovuti
ya serikali na ya Manispaa hiyo ya Kinondoni na nyingine zote
atakazotaka.
Mwenda amesema, baada ya kuweka mtandao kwenye Kituo hicho, mwakani Manispaa hiyo itaweka mtandao huo wa WiFi kwenye Kata zote 34 za Manispaa hiyo.
Amesema, mradi huo wa WiFi
umegharimu sh. milioni 21, na Manispaa hiyo itakuwa ikiendelea kulipia
huduma hiyo sh. milioni 2 kila mwezi ambazo itakuwa inalipa kwa mkupuo
kwa mwaka. Kuzinduliwa kwa huduma hiyo, kumeifanya Manispaa ya Kinondoni
kuwa ya kwanza nchini kote, na pengine hata Afrika Mashiriki, kutoa
huduma hiyo bure tena bila kutumia namba ya siri.
Huduma inayofanana na hii hupatikana katika nchi mbalimbali zilizoendelea dunian.Chanzo:Bongonewstz.com