Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA Imewataka wananchi wa mikoa ya Tabora na Singida kuepukana na dhana potofu ya matumizi ya televisheni walizonazo kuwa hazitumiki katika matangazo ya kidijiti bali waendelee na televisheni zao kwani king’amuzi hakina luninga maalum.
Hayo yamebainishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano na Utangazaji nchini Tanzania Bwana Fredrick Ntobi wakati akitoa taarifa ya kuzima mitambo ya analojia ifikapo tarehe 31 machi mwaka huu itakayohusisha maeneo ya mikoa hiyo.
Ntobi amesema kuwa utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwenye mitambo ya maeneo ya dijitali ambapo watoa huduma za kusambaza ving’amuzi walioko Tabora kuhakikisha kuwa kuna ving’amuzi vya kutosha.
Aidha wananchi wa mkoa Tabora wasizitupe tv zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya kidijitali.
Hata hivyo wakizungumza na vyombo vya habari baadhi ya wananchi wa mkoa wa Tabora wameonesha wasiwasi wao kuhusu mfumo mpya wa kidijitali wa upataji wa matangazo ya televisheni kwa kuwa watu wengi bado hawajanunua ving’amuzi na ambao wamenunua wanalamika kuwa baadhi ya chaneli hawazipati.