Saturday, July 5, 2014

MJERUMANI MBARONI KWA KUIFANYIA UJASUSI MAREKANI

Vyombo vya habari vinapasha kuwa, Maafisa nchini Ujerumani wanawashikilia Wajerumani wawili wanaoshukiwa kuifanyia ujasusi na kufanikisha kupenyeza taarifa za siri kwa maafisa wa Marekani, kwa hiyari yao wenyewe.
Steffen Seibert, Msemaji wa Chancellor Angela Merkel, amekiri kutaarifiwa kuhusu suala hilo lililotokea Jumatano ya wiki hii na kusema kuwa Chancellor Merkel alizungumza na Rais wa Marekani, Barack Obama siku ya Alhamisi (ijapokuwa
hakusema ni kipi kilikuwa kiini cha mazungumzo hayo).
Uhusiano baina ya mataifa haya mawili makubwa kiuchumi Duniani umetikiswa kutokana na kuvuja kwa siri za shirika (NSA) lililokuwa likidukua taarifa za mawasiliano nyeti duniani ikiwepo ya Wajerumani na kiongozi wao, Merkel.

Inasadikiwa kuwa mmoja wa waliotiwa mbaroni ni kijana wa umri wa miaka 31, mwajiriwa wa idara ya kiitelijensia ya mambo ya nje ya Ujerumani, aliyenyakua nyaraka za siri 218, ambazo aliziuza kwa $34,000 na kutuma taarifa za Bunge la Ujerumani (Bundestag) kuhusu udadisi wa aina ya maswali yanayokusudiwa kuulizwa ili kupata majibu kuhusu udukuzi wa NSA/Marekani kwa Ujerumani.

Awali, mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa kuhisiwa kuwa anafanyia ujasusi nchi ya Urusi lakini baadaye alikaririwa na chombo kimoja cha habari cha nchini Ujerumani kuwa alikiri kufanyia Marekani ujasusi.

Mtuhumiwa alifikishwa katika korti kuu huko Ujerumani na kuamuriwa kushikiliwa kwa dharura kwa kuwa na nyaraka za kiitelijensia bila ruhusa maalumu. 

Chanzo:http://www.wavuti.com

Popular Posts

Labels