Kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu imependekeza kwa serikali iongeze adhabu ya faini kutoka shilingi milioni tatu na kifungo kisichopungua miezi sita na kuwa faini ya shilingi milioni tano na kifungo kisichopungua miezi sita kwa wale wote watakaotuma katika mtandao taarifa za uongo.
Aidha kamati hiyo ilipendekeza katika adhabu kwa watu wanaonyanyasa wenzao kupitia mtandaoni adhabu yao iongezwe kutoka kifungo cha cha mwaka mmoja na kuwa kifungo cha miaka mitano.
Awali akiwasilisha maelezo ya muswada huo,Waziri wa Mawasilino,Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa alisema kutokana na kukua kwa matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano kumesababisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa makosa ya mtandao.
Alitaja makosa ya mtandao yaliyokithiri kwa sasa kuwa ni makosa dhidi ya faragha,usalamana upatikanaji wa taarifa za kompyuta na mifumo ya kompyuta,makosa yanayohusu maudhui,makosa dhidi ya mifumo ya kompyuta na makosa ya kawaida yanayofanywa kwa kutumia mitandao.
Profesa Mbarawa alisema kuwa takwimu kutoka jeshi la polisi zinaonesha kuwa makosa ya uhalifu wa mtandao yaliyoripotiwa na kuchunguzwa kati ya mwaka 2012 hadi Agosti mwaka jana ni 400.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2000 hadi mwaka 2013,makosa ya uhalifu wa mitandao yalisababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kwenye taasisi za fedha.