Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kutoa maoni yatakayoiboresha sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015 iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete ili yasaidie kuiboresha.
Imesema licha ya sheria hiyo kusainiwa na Rais, bado kuna umuhimu wa kuiboresha katika baadhi ya vipengele vyenye upungufu.
Kauli hiyo imetolewa Mei 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa (Pichani) katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake.
Mkutano huo uliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuufahamisha umma kuhusu kusainiwa kwa sheria hiyo na rais wa Tanzania na kuelezea umuhimu wake, huku pia waziri huyo akiitumia fursa hiyo kukaribisha maoni ya wadau mbalimbali kwa ajili ya kuiboresha.
“Tunaomba wananchi tuipokee sheria hii kwa sababu ni nzuri na itasaidia sana kuwalinda, lakini pia kama kuna kifungu chochote ambacho kitaonekana kuwa na upungufu leteni ushauri au maoni wizarani, tutayatafakari na tutayafanyia kazi,” alisema Mbarawa.
Waziri Mbarawa amesema Tanzania si nchi ya kwanza kupitisha sheria ya aina hiyo kwa sababu ya uwepo wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kulikosababisha kuongezeka kwa uhalifu wa mitandao.
Profesa Mbarawa amesema nchi za Uingereza, India, Malaysia, Uganda, Korea Kusini, Singapore, Mauritius, Afrika Kusini, Marekani na nyinginezo tayari zina sheria ya aina hii na inasaidia kuwapa wananchi haki wanapofanyiwa uhalifu wa mitandaoni.
Sheria ya Makosa ya Mitandao mwaka 2015 ni moja ya sheria zinazokosolewa na wadau wa habari pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii, kwa madai kuwa inalenga kubana uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kubinya uwanja mpana wa ukusanyaji na utoaji habari kwa waandishi wa habari.