Meneja
Uhusiano wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Thomas Mushi
akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam kukanusha
taarifa za kampuni hiyo kudukuliwa.
Meneja
wa Kitengo cha Usalama Mifumo ya Mawasiliano ya TTCL, Lina Rujweka
akifafanua jambo kwenye mkutano na vyombo vya habari.
Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL) imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa mfumo wa
mawasiliano wa kampuni hiyo umeingiliwa na wadukuzi. Taarifa iliyotolewa juma hili
kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Nicodemus
Thomas Mushi alisema taarifa zinazotolewa si za kweli hivyo kuwataka wateja wao
wazipuuze.
“Tunapenda kuwathibithia Wateja wetu wote
wa ndani na nje ya nchi, wadau wetu na Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si
sahihi, na kwamba mifumo yetu ya Mawasiliano ya TTCL ipo salama, huduma zetu
zote zipo thabiti na mpaka sasa tunapotoa taarifa hii, hakuna uhalifu wowote
uliofanyika kwa sisi wenyewe kama Kampuni wala kwa mteja wetu yeyote,” alisema Thomas
Mushi.
Aidha, tunapenda
kuwathibitishia kuwa, taarifa za Wateja wetu wote ikiwemo Serikali , Idara,
Wakala na Taasisi za Umma, Taasisi za fedha, Mashirika, Makampuni na Watu
binafsi zipo salama kabisa. Ukweli huu unathibitishwa na Wateja wao pia kwani
hadi sasa, hakuna hata mmoja aliyeleta taarifa za kukosa huduma ama kupata
athari zozote kutokana na tetesi hizo.
Hata hivyo, alisema
pamoja na taarifa hizo, Wataalamu wa kampuni hiyo wanaendelea kuwa macho kwa
muda wote, ili kuhakikisha kuwa, wanafanyia kazi kila taarifa ama tishio la
kiusalama linaloweza kujitokeza katika mfumo wao.
“TTCL inaendelea
kuwaomba Umma na Wateja wetu wote kuendelea na majukumu yao kama kawaida bila
wasiwasi wowote. TCCL inawaleta Karibu.” Alisema Thomas Mushi.
Kwa upande wake
Meneja wa Kitengo cha Usalama Mifumo ya Mawasiliano ya TTCL, Lina Rujweka
alisema kitengo chao baada ya tetesi hizo kimefanya uchunguzi wa kina na hakuna
ashirio lolote la mifumo yao kuingiliwa (kudukuliwa) kama ilivyoelezwa.
Alisema kitengo
hicho kina wataalam ambao muda wote wapo kazini kufuatilia ufanisi wa mfumo wa
mawasiliano wa kampuni yao hivyo kuwaondoa hofu wateja wao.
“Baada ya
taarifa hizo Kitengo cha Usalama wa Mifumo ya Mawasiliano ya Kampuni ya TTCL
kiliingia kazini ili kubaini ukweli wa taarifa hizo na kufanya majaribio ya
kitaalamu ili kuthibitisha usalama wa mifumo yetu. Baada ya utafiti wa kina na
majaribio ya kitaalamu, tunapenda kuwathibithia Wateja wetu wote wa ndani na nje
ya nchi, wadau wetu na Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si sahihi...”
alisema.