Miongoni mwa changamoto inayoonekana kwa sasa katika teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) ni suala la ulinzi katika mitandao,japo pia baadhi ya wanateknohama hawafahamu sheria na kanuni za kuisalam zinazotumika katika masuala mbalimbali ya teknohama na hasa katika suala la kujilinda kwa mtumiaji wa mitandao mbalimbali ya internet.
Juma hili yamejitokeza matukio mawili ambayo yaweza kuwa mfano wa kuyatumia katika hili kwanza ni Mama mmoja anaitwa Mama Matinde mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye wataalamu wa teknolojia wanaoingilia mifumo mbalimbali ya mawasiliano (hackers) ambao wameingilia anuania yake ya barua pepe bila yeye kufahamu na kuwasiliana na watu anaowasiliana nao na kuwaambia kuwa yuko safarini nje ya nchi na hivyo kapata matatizo wamtumie pesa wakati si kweli.
Blog hii imezungumza na kwa njia ya simu Mama Matinde na ameeleza kwa sasa yuko Burundi na si katika nchi ambayo mhalifu ameitaja,anasema toka jana hawezi tena kuingia kwenye email yake na hivyo imebidi atengeneze anuani nyingine ya barua pepe.
Matukio haya yamekuwa yakitumiwa sana na hawa wataalamu wa mifumo ya mawasiliano ya komputa katika kufanikisha uhalifu wa mitandao ili kujipatia fedha kwa udanganyifu fikiria akiwasiliana na rafiki zako 50 akawaambia kila mmoja amtumie 50,000 atakuwa na shilingi ngapi?
Tukio lingine ni taarifa ya Ridhiwani Kikwete ya machi 17,2013 ambayo imenukuliwa na mtandao jamii wa wanabidii inaeleza kuwa mojawapo ya mambo makubwa ambayo yamejitokeza siku za karibuni hasa katika suala la Teknolojia na habari ni jambo la sheria za faragha (privacy and privacy laws).
Ridhiwani anasema tumeshuhudia kufungwa kwa gazeti za News of The World, mali ya bilionea Rupert Murdoch wa Kimarekani baada ya kudhihirika alitumia wataalam wa teknolojia (hackers) kutafuta siri za watu mashuhuri kwa kuingia katika simu zao za mkononi kinyume cha utaratibu na sheria za faragha (Privacy Laws).
Anaeleza wahalifu hao hao wa mtandao wamekuwa wakifanya mengi kama kuvamia kwa mitandao ya makampuni makubwa kama Sony na mengineyo na hata katika mitandao hii ya kijamii upo wakati marafiki zako wanakwambia mbona umenitumia kitu kisichoeleweka, na baadaye kuja kugundua kwamba si wewe uliyefanya hivyo.
Ridhiwani anasema Tarehe 1, 8 na 9 mwezi huu wa Machi alikuwa Dar es Salaam kwa shughuli zake za kawaida kimaisha lakini ziko updates 5 zilifanyika kwenye wasifu wake wa facebook moja ikimhusu mwandishi wa habari Absalom Kibanda aliyepigwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa na hivyo kwenda kutibiwa nchini Afrika ya Kusini.
Ridhiwani katika taarifa yake hiyo anasema tarehe hizo mwezi huu wa Machi, wahalifu wa mtandao wakiwa eneo la Njiro na baadaye Kijenge mjini Arusha (Kila post ilionyesha eneo ilipotoka), (wakati huo yeye akiwa Dar es Salaam) waliingia bila idhini kwa njia haramu (Hacking) katika anuani yake ya Facebook na ku-post habari hizo tano.
Kutokana na matukio haya mawili yaani la Mama Matinde na hili la Ridhiwani Kikwete kuna changamoto kubwa sasa kwa watumiaji wa mitandao hasa masuala ya usalama katika mitandao,inashauriwa kuwa neno la siri la kuingilia katika anuani ya barua pepe inatakiwa liwe lenye mchanganyiko wa herufi na namba yaani liwe gumu kwa mtu kulibashiri baadhi huwa tunatumia miaka ya kuzaliwa na hivyo mtu aweza kubahatisha akaaingia bila wewe kujua ana akamua kufanya chochote bila mhusika halisi kujua,pia inashauriwa uwe unabadilisha neno hilo la siri kila baada ya miezi mitatu yaani usitumie neno moja la siri kwa muda mrefu.
Suala lingine ni kuhusu usalama katika mitandao jamii hasa facebook na twitter,skype ambazo zinaonekana kuwa na watumiaji wengi na zingine zimeunganishwa kwa maana ya kwanza unaweza kuwa na wasifu kwenye mitandao mitatu na unaingia kwa kutumia neno moja la siri ama ukishaingia kwenye mtandao mmoja wa kijamii moja kwa moja utakuwa umeingia kwenye mtandao mwingine kwa hiyo unaweza ukajisahau na mtu akatumia mwanya huo kuingia bila idhini yako.
Baadhi ya watumiaji wa facebook wamekuwa wakijisajili kwenye mtandao huo wa kijamii na kuonesha namba za simu na anuani zao za barua pepe wazi hili nalo sio jambo jema katika kujilinda na wahalifu wa mitandaoni ambao wanaweza kutumia mwanya huo kufanya lolote baya katika wasifu wako na kuonekana umefanya wewe ikiwa ni pamoja na kukuchafua ama kufanya uhalifu na kuonekana wewe ndo umefanya.
Kosa lingine ni kutoweka vizuizi vya faraga katika mitandao jamii ambavyo waundaji wa mitandao jamii wameiweka na kuifafanua lakini wengi wetu hatusomi ama hatuifahamu,juma lililopita wasifu mmoja wa kanisa la waadventista wasabato kwenye mtandao wa kijamii wa facebook mtu mmoja anayetumia jina la kike aliweka picha ya mwanamke akiwa uchi na picha hiyo ikaonekana katika wasifu huo wa kanisa mpaka blog hii ilipowasiliana na msimamizi wa wasifu huo ili kuiondoa picha hiyo chafu.
Bado kuna changamoto nyingine ya kutofahamu kujilinda hasa kwa watu wanaotumia simu za kisasa (smartphones) ambazo zina GPRS mfumo unaofanyakazi kwa simu za kisasa kama kuna mawasiliano ya internet ambayo inaweza kuonesha mahali ulipo kama umeiweka on hasa kama unaweka pachiko ama unawasiliana na mtu kwenye mtandao jamii kama vile facebook.
Bado kunahitajika utoaji wa elimu ya teknohama kwa jamii hasa nchini Tanzania.Kwa maelezo zaidi waweza kuendelea kusikiliza kipindi cha maisha na tekhohama Morning Star Radio kila jumapili saa 3:00 asubuhi.MOROGORO 98.9 FM,MWANZA 102.1FM, MUSOMA 98.9 FM, KIGOMA 103.3 FM, ARUSHA 102.5 FM, MBEYA 106.9 FM na DAR ES SALAAM 105.3 FM.
1
3