Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) inatarajia kutoa huduma katika maeneo ya vijijini kwa gharama ya shilingi bilioni tatu na nusu.Taarifa ya ushindi wa zabuni wa kampuni hiyo iliyotolewa leo katika vyombo vya habari inaonesha kuwa TTCL itatoa huduma za mawasiliano katika kata 20 zenye jumla ya vijiji 103 na jumla ya wakazi zaidi ya 160,000 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Mradi huu ni wa kitaifa wenye lengo la kusaidia maeneo yasiyokuwa na huduma za mawasiliano kwa muda mrefu sasa.Mradi ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha kuboresha huduma za mawasiliano vijijini,ambacho kipo chini ya Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia.
Vijijini husika vya mradi huu viko katika mikoa 10 ambayo ni Arusha,Manyara,Dodoma,Lindi,Mbeya,Morogoro,Mtwara,Ruvuma,Shinyanga na Tanga.
Huduma zitakazotolewa katika mradi huu ni simu yaani maongezi,huduma za ujumbe mfupi (sms) na mtandao wa internet zote kwa teknolojia mchanganyiko za mkongo na isiyokuwa na waya.