Wamiliki wa vituo vya utangazaji vya televisheni nchini,
wamesema watasitisha kurusha matangazo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa
kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
Hatua hiyo inatokana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali Desemba 31, mwaka jana kitendo walichodai kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi alisema hakuna haja ya kurusha matangazo kwa hasara.
Mengi alisema kutokana na kuanza kwa mfumo wa dijitali, watangazaji wamesitisha kutoa matangazo kwa sababu wananchi wengi hawana ving’amuzi.
Kama mamlaka itashindwa kurudisha ule mfumo wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi wananchi watakapokuwa na ving’amuzi, tutazima televisheni zetu ndani ya mwezi mmoja ujao,” alisema Mengi.
“Ibara ya 18 ya Katiba imekiukwa kutokana na wananchi kunyimwa fursa ya kupata habari, hivyo hali hii hatutaki iendelee,” alisema Mengi.
Mengi ambaye pia ni mmiliki wa vituo vya televisheni vya ITV, EATV na Capital TV, alisema licha ya nchi za Afrika, Tanzania imekuwa ya kwanza kuzima mitambo ilhali wananchi hawakuwezeshwa kumudu gharama za ving’amuzi.
“Nchi ambazo zimeendelea kwa kila kitu kama Uingereza, Marekani, Japan na kwingineko kuzima mitambo ya analojia walitumia zaidi ya miaka minane kwa nini sisi tumewahi hivi wakati hatujajipanga?” alihoji Mengi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Media Group na mmiliki wa Kituo cha Star Tv, Samwel Nyalla alisema hivi sasa wanaendesha biashara hiyo kwa hasara.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi