Jeshi la
Polisi mkoani Dodoma, limemkamata mkazi wa Chang’ombe mkoani humo Noel
Mlingwa (25), kwa tuhuma za kumtumia ujumbe mfupi wa matusi kwa njia ya
simu, Spika wa Bunge Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai. Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, alitoa taarifa hiyo jana kwenye vyombo vya habari. Alisema mtu huyo alikamatwa Februari 12, mwaka huu, eneo la Shule ya Sekondari ya City iliyopo Area A.
Alisema
mtuhumiwa huyo ambaye amekana mashtaka hayo alifikishwa katika Mahakama
ya Wilaya ya Dodoma Mjini, juzi na kesi yake imeahirishwa hadi Machi
21, mwaka huu itakapotajwa tena.
Kamanda
Misime aliwataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuacha kutumia simu zao za
mkononi kwa kutuma ujumbe wa matusi na vitisho kwa watu wengine.
Alisisitiza kuwa atakayekamatwa kwa tuhuma hizo atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Kutukanwa
kwa viongozi hao wa Bunge, kulifuatia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kutangaza namba za Spika na Naibu wake katika mkutano wa
hadhara uliofanyika jijini Dar es Salaam ili wawashinikize wajiuzulu.
Siku moja
baada ya mkutano huo, chanzo kilicho karibu na Spika Anne Makinda ,
kilisema jumla ya simu 200 zilipigwa kwa ajili ya kumtukana.
Hali
kadhalika katika kipindi hicho jumla ya ujumbe mfupi 400 wa simu za
mkononi (SMS), uliokuwa ukimtukana ulipokelewa katika simu zake.
chanzo:chingaone blog