Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeingilia kati wizi wa fedha kwa kutumia mashine za kutolea fedha (ATM), ambao umeibua hofu kubwa katika sekta ya benki nchini.
Kutokana na wizi huo kukithiri katika baadhi ya benki, wafanyabiashara na wananchi wameanza kujipanga kuondoa fedha zao katika akaunti.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu alizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki kwamba wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.
“Wizi kama huo unatokea wakati mtu anaweka namba za siri kwenye ATM kwani kuna watu huweka kamera ambazo husoma na namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha kufanya wizi ,” alisema Profesa Ndullu.
Alisema kuwa kutokana na wizi kukithiri wamezitaka benki zote kuweka mifuniko katika eneo la namba za siri ili wezi wanaoweka kamera ili kuzinasa wakati mtu anatoa fedha washindwe kufanya hivyo.
Profesa Ndullu alisema wanafuatilia mfumo wa utendaji wa benki ili kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa limeibua mijadala na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Benki kubwa nchini zimekumbwa na mtikisiko wa wizi wa fedha kwa kadi za ATM, ambao umeongezeka kwa kasi kiasi cha kufanya wananchi wengi kuhifadhi fedha zao kwenye mitandao ya makampuni mbalimbali ya simu za mikononi ambayo hata hivyo ripoti zimekuwa zikieleza kuwa nako usalama wake si wa kiwango cha juu.
Baadhi ya benki ambazo zimekumbwa na matukio hayo zimekuwa zikisita kutoa taarifa kueleza sababu za kushindwa kuzuia wizi huo na badala yake zimekaa kimya kuhofia kupoteza wateja.
Kukua kwa teknolojia za kifedha ambako kumerahisisha ufanisi wa matumizi na utunzaji wa fedha, sasa kunaonekana kugeuka na kuwa balaa kutokana na kuibuka kwa wizi mkubwa mahala zinakohifadhiwa kwenye akaunti za wateja kwa kutumia njia ya mtandao.
Taarifa za wizi huo zilianza kurindima mwezi Machi, 2010, ambako kiasi cha mabilioni ziliibwa kupitia katika mashine za ATM huku kati ya kiasi hicho jumla ya Sh360 milioni zikihusisha benki moja nchini.
Hata hivyo, mwaka huo watu wanne walikamatwa baada ya kuripotiwa wizi huo mkubwa. Sambamba na kukamatwa kwa watu hao, pia alikamatwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akifanya jaribio la kuiba kimafia Sh221 milioni kutoka benki ya NBC.
Wimbi la wizi huo limeibuka tena katika kipindi cha Oktoba 2012 hadi Februari 2013 na inakadiriwa kuwa jumla ya kiasi cha Sh700 milioni kimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi