Ofisa Biashara wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Thomas Lemunge akitoa ufafanuzi katika semina kwa wahariri juu ya mkongo wa taifa katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam |
Vyombo vya habari nchi vimeombwa
kutoa elimu kwa jamii juu ya manufaa ya uwepo wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
(National ICT Broadband Backbone-NICTBB) ili wananchi wauelewe na kuulinda
kutokana na umuhimu wake.
Changamoto hiyo imetolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam naMeneja
Uendeshaji wa NICTBB, Adin Mgendi alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo
anuai vya habari juu ya utendaji kazi wa mkongo huo na manufaa yake kwa taifa.
Mgendi alisema manufaa ya ujenzi wa Mkongo wa mawasiliano nchini yameanza
kujitokeza hivyo Watanzania wana kila sababu ya kuulinda mtandao huo kwani
unaumuhi mkubwa kwa jamii na taifa.
Alisema kwa sasa jumla ya nchi sita, ambazo ni pamojana Malawi, Zambia,
Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya zimeunganishwa na Tanzania hivyo nchi yetu
ikibeba dhamana ya kuwahudumia kupitia mtandao wa Mkongo.
Mtalamu huyo alivitaka vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa wananchi
hasa waliopo karibu na njia ya mkongo ili wasiuharibu kupitia shughuli
mbalimbali za kijamii zinazofanyika ardhini.
Akifafanua zaidi kwa wahariri wao, Ofisa Biashara wa Mkongo, Thomas Lemunge
alisema kwa sasa mikoa yote ya Tanzania Bara tayari imeunganishwa na mkongo
hivyo kurahisisha miundobinu ya mawasiliano.
Aidha aliongeza kuwa mtandao wa mkongo ambao ujenzi wake uaendelea umepita
maeneo anuai; ikiwemo ardhini pembezoni mwa barabara, mashambani, juu ya nyaya
za umeme na kwenye maji huku ukiwa na mizunguko mitatu yaani wa Kaskazini,
Magharibi na Kusini.
Awali akizungumza na washiriki hao, kabla ya kufungua warsha hiyo,
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini (TEKNOHAMA), Mhandisi
Zaipuna Yonah alisema mkongo unamanufaa makubwa kwani hadi sasa matumizi ya
intaneti yameongezeka tofauti na awali.
“Ongezeko la matumizi na faida za mkongo zinaongezeka siku hadi siku na
hivyo kukidhi matarajio ya Serikali ya kuziba pengo la matumizi ya TEKNOHAMA
kwa wananchi katika maeneo ya mbalimbali ya nchi yetu na hatimaye kukuza
uchumi,” alisema Yonah.
Wahariri hao walipata fursa ya kutembelea kituo kikuu kinachoratibu shughuli
za mkongo maeneo mbalimbali ya nchi na kuona namna wataalamu wanavyofanya kazi
eneo hilo.
Mkongo wa taifa ambao kwa sasa unategemewa na nchi jirani za Tanzania na makampuni binafsi katika usabazaji huduma za mawasiliano unasimamiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) huku wakiwa ndio meneja wa Mkongo huo.
Chanzo:The Habari.com