Watu wasiofahamika wameukata Mkongo wa Taifa kati ya Masasi na Mchinga mkoani Mtwara.Mkongo huo wa taifa ambao ni miundo mbinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano,uligunduliwa kukatwa kupitia kituo chake cha kikuu cha kuongozea kilichopo jijini Dar es salaam.
Mmoja wa wahandisi wa Mkongo wa Taifa,Isaji Mwamkonda aliwaambia wahariri na waandishi wa habari waandamini kituoni hapo jana kuwa, bado haijafahamika kama kitendo hicho ni cha hujuma ama la.
Hata hivyo,Mwamkonda alisema wahandisi kutoka katika kituo cha Mtwara,tayali wamefika kwenye eneo la tukio na walikuwa wakiendelea kufanya tathimini kubaini chanzo halisi cha uharibifu huo.Aidha alisema tathimini hiyo pia itasaidia kufahamu kazi ya kuurekebisha itachukua muda gani.
Mhandisi huyo alisema kukatwa kwa mkongo huo katika eneo hilo,hakutaathiri mawasilino kwa mkoa wa Mtwara kutokana na muundo wake wa kitaalamu.
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa iwapo watabaini watu wanaoharibu kwa makusudi Mkongo wa Taifa kwa kupiga simu bila malipo namba 144 ama 0800115555 kwa mitandao yote.
Kampuni ya simu ya nchini Tanzania (TTCL) ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano,kutunza na kuendesha shughuli zote za ufundi na kibiashara zinazotokana na kukodisha njia zake zenye kasi kubwa ya kusafirisha mawasiliano kwa kampuni zinazotoa huduma kwa taasisi na wananchi kwa maendeleo.
Kampuni hiyo pia imepewa jukumu la kuendeleza mkongo huo kwa kuusambaza nchi nzima,Kwa sasa mkongo wa taifa umesambazwa katika kilomita 7,560 kwenye mikoa yote Tanzania ambapo kati ya kilomita 2,088 mkongo huo umepitishwa katika nguzo kubwa za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na zilizobaki zimechimbiwa ardhini.