Tuesday, February 12, 2013

MAKINDA ASHAMBULIWA KUPITIA SIMU

Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda

Gazeti  la Nipashe toleo la leo limeandika kuwa Baada ya  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza namba za Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, katika mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu wamezitumia kumtukana Makinda.
 
Chanzo kilichopo karibu na Spika kimesema kuwa tangu chama hicho kilipotangaza namba hizo za simu, jumla ya simu 200 za kumtukana Spika zilipigwa.
 
Hali kadhalika, katika kipindi hicho jumla ya ujumbe 400 mfupi wa simu za mkononi (sms), uliokuwa ukimtukana ulipokelewa katika simu zake.
 
“Simu hizo walikuwa wameshika wasaidizi wake, kila aliyepiga simu kwa lengo la kutukana, amekuwa akiachwa kutukana hadi anapomaliza na kisha kuambiwa sawa,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake liandikwe gazetini.
 
Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta Spika Makinda jana kuzungumzia suala hilo bila mafanikio na kuelezwa kuwa ofisi ya Bunge itafanya mkutano na waandishi kati ya leo ama kesho kulizungumzia sakata hilo.
 
 Viongozi wa Chadema waligawa namba za viongozi hao wa juu wa Bunge Jumapili iliyopita katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam.
 
 
 

Popular Posts

Labels