Picha kwa hisani ya http://www.earthisland.org |
Watuamiaji wa simu za mkononi nchini
Kenya,Rwanda na Uganda hivi karibuni watakuwa wakipiga simu kwa bei
nafuu,baada ya wahudumu wa simu kukubaliana kupunguza ada ya kupiga simu
katika eneo lolote la Afrika Mashariki.
Waziri wa mawasiliano nchini Kenya amesema kuwa watumiaji wa simu za mkononi watalipa ada za chini ili kupiga simu katika mtandao wowote katika taifa la Afrika ya Mashariki.
Wale walio katika mataifa hayo hawatalipishwa kwa kupokea simu.
''Tumepunguza ada ya kupiga simu katika eneo la Afrika Mashariki'',alisema waziri Fred Matiangi.
Kenya Rwanda na Uganda ni mataifa matatu kati ya matano ambayo yanaleta pamoja jumuiya ya Afrika Mashariki,inayolenga kupunguza vikwazo vya kibiashara .
Inatarajiwa kwamba wanachama wengine wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania na Burundi pia watatekeleza mpango huo,ili kuwashinikiza wahudumu wa simu katika mataifa hayo mawili kupunguza ada ya wateja wao kupiga simu wanapokuwa katika mataifa mengine ya afrika mashariki.
Nebert Rugadya ambaye ni mchambuzi wa maswala ya kiuchumi nchini Uganda ameiambia BBC kwamba ada ya kupiga simu kutoka mataifa mengine ya afrika mashariki ni ya juu mno.
''Kupiga simu nchini Kenya kutoka Uganda imekuwa ikigharimu shilingi 2000,lakini iwapo ada ya kupidga simu katika taifa lolote la Afrika Mashariki itapunguzwa basi simu hiyo itagharimu shilingi 260'',alisema Rugadya.
Hatua hiyo itapunguza gharama ya mawasiliano katika eneo hili mbali na gharama ya biashara.
Chanzo:BBC