Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imeeleza kujivunia mabadiliko ya utumiaji wa Teknohama katika utendaji wake wa kazi katika kipindi cha miaka saba iliyopita ndani ya idara hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Majukumu ya idara hii ni kuwezesha kudhibiti ujangili,utokaji wa watu na ukaazi wa wageni nchini Tanzania,kutoa huduma ya hati za kusafiria na hati nyingine za safari kwa raia wenye sifa na kuratibu mchakato wa maombi ya uraia wa Tanzania kwa wageni wanaoishi nchini Tanzania kihalali.
Moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika kuboresha utoaji wa huduma za uhamiaji ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.Kati ya mwaka 2006 na 2012,idara hii imefanikiwa kuboresha utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya komputa na mitandao yake katika utoaji wa huduma.
Jumla ya Mifumo minane imefungwa na inaendelea kutumika katika utoaji wa huduma katika sehemu tofauti tofauti za idara hii.
Kwanza mfumo wa utoaji wa hati za kusafiria huu ulifungwa mwaka 2005 katika ofisi za makao makuu ya uhamiaji Dar es salaam na Zanzibar huu unatumika katika kutoa hati za kusafiria kwa wananchi wa Tanzania,Mwingine ni mfumo wa utoaji wa Viza ambao unahusika na utoaji wa visa kwa wageni wanaohitaji kuja Tanzania pamoja na kutunza kumbukumbu zao ambao ulifungwa mwaka 2006 katika balozi 33 za Tanzania nje ya nchi na katika vituo vikubwa 19 vya kuingia na kutoka Tanzania.
Mfumo mwingine ni wa udhibiti na kutunza kumbukumbu za wasafiri ambao umefungwa mwaka 2003 na uliboreshwa mwaka 2010 ili kuongeza uchukuaji wa taarifa nyingine muhimu za wasafiri.
Pia kuna mfumo wa kudhibiti na kutunza kumbukumbu za wasafiri ambao umefungwa mwaka 2008 katika vituo 13 kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wasafiri na umeunganishwa na makao makuu ya mikoa na makao makuu jijini Dar es salaam.
Pia idara ya Uhamiaji ina mfumo wa utunzaji wa majalada,huu ulifungwa mwaka 2007 makao makuu ya uhamiaji na unatumika kutunza kumbukumbu za majalada kwa njia ya kielektroniki.Baada ya mfumo huu kuna mwingine ambao unahusika na utoaji wa vibali vya ukaazi ambao ulifungwa mwaka 2012 makao makuu ya idara hiyo jijini Dar es salaam na Ofisi Kuu ya idara hiyo huko Zanzibar,huu ni mfumo ambao unatumika kuchapisha vibali na kutunza kumbumbu za wageni wanaoomba kuishi Tanzania japo bado unahitaji maboresho ili ulete mafanikio.
Kuna mfumo wa kutoa vyeti vya uraia wa Tanzania kwa wakimbizi 2009 huu huhusika kusimamia wanaoomba huduma nao umefungwa yalipo makao makuu mwaka 2012 huu ni kwa ajili ya kusimamia utoaji huduma kwa kujali muda aliofika mteja,huu umerahisisha ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi wa maofisa wanaohudumia wateja.
Taarifa ya idara hiyo inaonesha kuwa hadi kufikia Desemba 2012 ilikuwa imetoa hati za kusafiria 537,426 kati ya hizo hati za kusafiria za kawaida ni 518,561,za kidiplomasia 4753,za kiutumishi 1499 na hati za kusafiria za Afrika Mashariki 12,613.
Kati ya mwaka 2006 hadi Desemba 2012,Waziri wa Mambo ya Ndani amekubali maombi ya wageni 1,027 walioomba uraia wa Tanzania..