Serikali ya Tanzania
inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa hivi karibuni kumezuka
kundi la Watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi
waandamizi wa serikali na Taasisi nyeti ikiwemo Usalama wa Taifa
kujipatia fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi hao.
Watu
hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwa maofisa mbalimbali
wa wizara, mashirika ya umma na Idara za Serikali zinazojitegemea
kuomba pesa ili wawafanye mipango ya kupandishwa vyeo.
Utapeli
huo umekuwepo nchini kwa kipindi kirefu sasa, ambapo watu huwapigia
simu viongozi wa Taasisi za fedha, Mifuko ya Taasisi za Jamii na watu
binafisi wakiomba fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi waandamizi
Serikalini wakati si kweli.
Watu
hao wamekuwa wakiwatapeli maofisa mbalimbali kuwa wanaweza kuwafanyia
mipango ya kupandishwa vyeo endapo watawapatia kiasi cha fedha jambo
ambalo halipo katika taratibu za utumishi wa umma.
Utumishi
wa umma unazo taratibu zake za kuwapandisha vyeo watumishi wake
kulingana na sifa za kada zao na wala haiwezekani kwa viongozi
waandamizi kuwachangisha fedha kwa ajili ya kuwapandisha vyeo. Serikali
inawataka wananchi kuwapuuza matapeli hao na watoe taarifa katika vyombo
vya dola na usalama mara wapatapo ujumbe wa aina hiyo ili hatua
zichukuliwe dhidi yao.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
DAR ES SALAAM.
12.02.2013
Chanzo:wanabidii googlegroups.com