Utafiti uliofanywa mwaka jana na Kampuni ya Utengenezaji wa simu ya Nokia kabla haijabadilishwa na kuwa Microsoft kuhusu biashara ya mauzo ya simu katika nchi mbalimbali barani Afrika,Tanzania ikiwa ni miongoni mwao,umebaini kuwa kuna mianya ambayo imekuwa ikitumika kuingiza simu hizo kwa njia za magendo bila kulipia ushuru huku ukiikosesha Serikali ya Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 91.23.
Utafiti huo unaeleza kuwa njia ambazo zimekuwa zikitumika ni upitishaji wa simu katika maeneo ya pembezoni mwa nchi hususani mikoa iliyoko mipakani mwa Tanzania na nchi jirani na kuingiza simu za magendo kupitia katika viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam na ule wa Kilimanjaro ambapo wafanyabiashara hulipia kiasi kidogo cha fedha ambazo hukadiliwa bila kuangalia uzito na thamani ya mzigo alionao.
Takwimu za utafiti huo zinaonesha kuwa kwa wastani,simu za kawaida takribani 750,000 huuzwa kwa mwezi nchini Tanzania ambapo wastani wa bei kwa simu moja ni Sh 35,000 ambapo jumla ya mauzo ni Sh bilioni 26.2,huku kwa upande wa simu za kisasa kwa mwezi zikiuzwa simu 87,000 na wastani wa bei ikiwa ni Sh 250,000 ambapo mauzo yake kwa mwezi ni sawa na Sh bilioni 21.75.
Jumla ya simu zinazouzwa kwa mwezi ni 837,000 ambapo thamani yake ni Sh Bilioni 48,kama zimu zote zitalipiwa ushuru wa asilimia 18 na mianya yote kufungwa basi serikali inastahili kukusanya Sh.Bilioni 8.64 kwa mwezi.