Friday, November 15, 2013

TCRA - WANAOVUJISHA MAWASILIANO YA WATU WASHITAKIWE

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni za simu za mikononi, zimewataka wateja watakaokumbwa na tatizo la kuvujishwa kwa taarifa za simu, kuripoti kwenye vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe.

Aidha imeelezwa kuwa ingawa kumekuwa na mashine za kuzuia taarifa za siri za simu za mikononi kutovuja, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu wateja kinyume cha sheria kwa kuchezea teknolojia isivyopaswa.

Hadhari hiyo imekuja kukiwa na wimbi la matumizi mabaya ya simu za mkononi nchini Tanzania, ikiwemo matumizi ya teknolojia kutoa 
hadharani mawasiliano ya siri ya watu.

Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni, ni taarifa zilizoanikwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Kabwe Zitto, zikionesha mawasiliano ya siri anayodaiwa kufanya na watu mbalimbali yakidaiwa kuwa ni ya kuhujumu chama chake.

Matumizi mengine ni aliyodai kufanyiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, ambapo pamoja na namba za simu kadhaa kudai zinamtumia ujumbe wa matusi, pia alidai upo ujumbe wa matusi unaotumwa kwa watu na namba inayojitokeza ikionesha ni ya mbunge huyo suala alilosema juzi limemchafua kisiasa na kijamii.

Akizungumza jana na mwandishi juu ya matukio hayo, Meneja Uhusiano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema kampuni za simu zinaongozwa kwa mujibu wa sheria hivyo hakuna itakayokubali kutoa taarifa za siri za mteja kwa kuwa ni hatari kwao.

Sheria husika ni ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 inayotoa kinga kwa mteja.

“Ninachojua ambacho kinaweza kuonekana na kupatikana kutoka katika kampuni hizo tena kama zikiombwa na Polisi ama vyombo vya usalama kufanya hivyo kwa kulinda usalama wa taifa, ni kuelezwa siku fulani uliwasiliana na nani na saa ngapi na kampuni zinaweza kuchapa taarifa hiyo na kuitoa bila kueleza kilichozungumzwa wazi wazi,” alisema Mungy.

Mungy alisema kampuni za simu zina utaratibu wa mafundi wake kuingia chumba cha kuhifadhi taarifa za siri, na ikiwa mtu ana uhakika namba ya kampuni fulani imetumiwa visivyo, anapaswa kutoa taarifa Polisi ili hatua zichukuliwe kwa kuwa hilo ni kosa la uhalifu wa mtandaoni.

“Naomba ieleweke kwamba haiwezekani mtu asikilize maongezi ya mtu na mtu, ama kusoma ujumbe mfupi wa simu za mkononi, ingekuwa hivyo wafanyabiashara wakubwa wasingefanya biashara wala taarifa za ulinzi na usalama wa nchi zisingekuwa siri leo, watu waondoe hofu na ikiwa mtu katendewa hivyo kweli, aende Polisi kupata haki yake,” alisisitiza Mungy.

Ofisa Mawasiliano wa Kampuni ya simu ya Zantel, Monica Ekelege akizungumzia suala hilo, alisema mafundi katika kampuni za simu wana uwezo wa kuona mawasiliano ya mtu na mtu ikiwa wanatafuta kitu na kujua namba ya mtu, lakini hawawezi kutoa mawasiliano hayo kwa kuwa kampuni nyingi zina mashine ya kuzuia siri.

“Huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine, mtu anaweza akachokonoa chokonoa na kuibuka na njia nyingine ya kuvujisha taarifa za mtu, huyu akibainika, sheria haimwachi lakini kwanza kwa kuwa sisi tunafanyakazi chini ya sheria inayomlinda mteja na siri zake, ana mamlaka ya kutushitaki lakini lazima awe na uthibitisho na kuanzia Polisi,” alisema Ekelege.

Ekelege alisema uhalifu mwingi wa simu wanaoufanya watu, wanatumia udhaifu wa baadhi ya mawakala waliozembea kutumia vielelezo stahiki katika kusajili namba za simu, na sasa baadhi wanatumia mwanya huo kufanya uhalifu.

Kuhusu watu wanaotumia simu kutuma ujumbe wa matusi au kufanya uhalifu mwingine kama vile utapeli, Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema mara nyingi wanaofanya vitendo hivyo ni wenye simu ambazo hazijasajiliwa kwa kufuata utaratibu unaopaswa.

Alisisitiza waathirika wa vitendo hivyo kutoa taarifa Polisi na kampuni yao itatoa ushirikiano kubaini wahusika ili hatua zichukuliwe.

Popular Posts

Labels