Kanisa la River Side lililopo mtaa wa Njiro jijini
Arusha, Tanzania, limetangazwa kuwa ni kanisa pekee barani Afrika ambalo
limefikia asilimia 80 ya kutunza kumbukumbu za majina ya washiriki kwa kutumia
mfumo wa kiteknolojia ya habari na mawasiliano wa usimamizi wa makanisa ya kiadventista.
Taarifa
hiyo imetolewa na Msimamizi mkuu wa
mfumo wa Usimamizi wa makanisa ya kiadventista duniani Mrs Sherri
Ingram-Hudgins Februari 9, mwaka huu wakati akitoa takwimu za mfumo mpya wa
kanisa la Waadventista wa kusimamia makanisa (ACMS) kwenye mkutano wa
wanateknohama wa kanisa hilo uliofanyika Maryland,Silver Spring,Marekani.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa Brazil ndio inaongoza duniani kuwa na
washiriki wengi waliosajiliwa, ikifuatiwa na nchi za Peru na Argentina. Barani
Afrika, Tanzania ndio inaongoza ikifuatiwa na Ghana.
Mwaka 2015, mfumo huu unategemewa kuanzishwa katika
nchi za Kenya, Africa Kusini na Madagascar.
Akieleza mbele ya wajumbe kutoka division 13 duniani, Sherri alionesha jinsi mfumo huu wa kusimamia makanisa ulivyoboreshwa kwenye vipengele 5 ambapo unauwezo wa kutunza kumbukumbu za vikao vya kanisa mahalia, kupiga kura za kuchagua viongozi wa kanisa, unawezesha kanisa mahalia kuufasiri kwa lugha husika ya kanisa mahalia ,kutunza kumbukumbu za fedha za kanisa na kukusanya taarifa za kila idara kisha kuzituma konferensi, unioni, divisheni na Konferensi Kuu.
Awali mfumo huu ulipoanza kutumika ulikuwa na uwezo wa
kutunza majina ya washiriki na kuhamisha jina la mshiriki toka kanisa moja
kwenda jingine.
Sherri ametoa rai
kwa wajumbe wote kuusimamia mfumo huu kwa makanisa yote makubwa yaliyopo mijini
kisha kwenda makanisa yaliyopo vijijini.
Divisheni ya Afrika mashariki na kati iliwakilishwa na
wajumbe watatu, Nicolas Washington (Kenya), Kelvin Opiyo (Kenya) na Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Unioni Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania Gideon Msambwa.