WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa, amesema uchumi wa Tanzania unaweza kukua kati ya asilimia mbili hadi tatu katika kipindi cha miaka michache ijayo iwapo itaipa kipaumbele sekta ya teknolojia ya mawasiliano na habari.
Mbarawa alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Techno Brain Tanzania na kuongeza kuwa Tanzania itafaidika na sekta hiyo hasa baada ya kuwekeza kwenye miundombinu (mkongo wa mawasiliano).
Alisema mpaka sasa mikoa 19 imeunganishwa pamoja na wilaya 57 na kusema kuwa hadi kufikia Machi mwakani, mkongo huo utakuwa umefikia kilomita 10,000.
“Lugha ya Kiingereza ni kikwazo kikubwa katika matumizi ya teknohama, hivyo tukiwa na mfumo wa teknolojia ya habari uliotafsiriwa kwa Kiswahili, itakuwa vizuri. Kampuni kama Techno Brain ikishirikiana na sisi katika hili, ndoto zetu zitafikiwa,” alisema.
Awali, Meneja wa Biashara wa Techno Brain, James Mungai, alisema kampuni yake tayari imefanya kazi mbalimbali na serikali ikiwemo Mfuko wa Hifadhi wa Taifa (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na kitengo cha Uhamiaji.