Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam wamezungumzia utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi na kusema wengi wanaofanya hivyo husajili laini kwa majina ya uongo.
Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es salaam,Ahmed Msangi amehadharisha wananchi kwa kutaka kuwa makini katika kutuma fedha kwa njia ya simu.
Alikuwa akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo juu ya utapeli uliohusisha kampuni ya ndege ya kimataifa ya Qatar ambao baadhi ya watu wameibiwa pesa zao baada ya kuzituma kwa watu waliojifanya ni maofisa wa kampuni hiyo kwa ahadi ya kupatiwa kazi.
Kaimu meneja Mawasiliano Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA,Semu Mkwakanjala anasema alisema wanafanya mikutano kadhaa na kampuni za simu za mikononi kukumbusha kufuata utaratibu wa usajili wa namba unaozingatia sheria ili kuepusha kuendelea kutokea kwa uhalifu kupitia simu za mkononi.