Friday, June 14, 2013

BAJETI:HUDUMA ZOTE ZA SIMU NCHINI TANZANIA KUANZA KUTOZWA KODI MWEZI UJAO


 

Wamiliki wa simu nchini kuanzia mwezi ujao wataanza kuingia gharama zaidi kwa asilimia 14.5 ili kuongeza mapato ya Serikali na kugharimia elimu. 

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.

Akifafanua suala hilo kama chanzo kipya cha mapato ya Serikali, Dk Mgimwa alisema Serikali inakusudia kuanzia mwezi ujao kutoza ushuru wa bidhaa wa kiwango hicho kwenye huduma zote za simu za kiganjani, badala ya muda wa maongezi peke yake.

“Katika ushuru huu, asilimia 2.5 zitatumika kugharimia elimu hapa nchini... Hatua hii imezingatia mapendekezo ya Kamati Maalumu ya Spika ya Kushauri kuhusu mapato na matumizi ya Serikali,” alisema Dk Mgimwa.

Kama vile haitoshi, Waziri Mgimwa alitangaza kuongeza wigo wa kutoza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za simu za mezani (zinazojulikana kama za TTCL) na zisizokuwa na waya.

Pia waziri alitangaza kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi. Kodi hiyo itakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa huduma za kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi;

Mapendekezo hayo ya Waziri Mgimwa ni utekelezaji wa ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itafute vyanzo vipya vya kodi ili kuongeza mapato ya Serikali. 

Miongoni mwa maeneo ambayo Ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, mwaka jana ilishauri kuangaliwa, ni pamoja na huduma za kuhamisha fedha kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na Easy Pesa.

CAG alishauri kuwa kampuni za simu kulipa kodi ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya biashara hiyo na kodi hiyo ya zuio ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho itakayotakiwa kulipwa na kampuni za simu.
Chanzo:Gazeti la mwananchi

Popular Posts

Labels