Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Habari na Elimu kwa Umma wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Cosmas Mwaisibwa akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya bodi na kampuni ya Vodacom Tanzania kuangalia namna ya kuimarisha na kuboresha zaidi uhusiano wa biashara baina ya taasisi hizo mbili. Wengine pichani kutoka kulia ni Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim na Naibu Mkurugenzi wa Tehama wa bodi Cuthbeth Simalenga. |
Bodi ya mikopo ya elimu ya juu Tanzania – HESLB imesema huduma ya M-pesa inayowawezesha waombaji wa mikopo ya elimu juu kwenye bodi hiyo kulipia ada ya uombaji kwa kiasi kikubwa imesaidia kurahisisha uendeshaji ikiwemo usimamizi na ufuatiliaji wa malipo hayo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini Bw. Cuthbeth Simalenga wakati wa kikao cha urafiki mwema kati ya uongozi wa Bodi na Kampuni ya Vodacom kilichofanyika makao makuu ya bodi hiyo yaliyopo Msasani Jijini Dar es salaam kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa taasisi hizo.
Bw. Simalenga amesema bodi hiyo ilianza kutumia huduma ya M-pesa kwa malipo ya ada ya maombi miaka mitatu iliyopita na kwamba tangu wakati huo huduma hiyo imekuwa ikiimarika na kutoa tija zaidi kwa upande wa uendeshaji wa shughuli za uombaji wa mikopo.
“Kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tukitumia huduma ya M-pesa kukusanyia ada za malipo ya maombi ya mikopo, kwa sasa waombaji wote wanatumia huduma hii na tumekuwa tukiboresha mifumo yetu ya ndani mara kwa mara kukabiliana na changamoto za hapa na pale zinazojitokeza.”Alisema Bw. Simalenga
Zaidi ya waombaji 50,000 wakiwemo waombaji wapya na wale wanaaondelea na elimu ya juu hutuma maombi ya mikopo kwenye bodi hiyo kwa mwaka, na wote kwa sasa wanatumia huduma ya M-pesa kulipia ada ya malipo ya maombi ambayo ni Sh 30,000.
Bw. Simalenga amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa katika mfumo huo wa malipo kuwa ni uaminifu wa waombaji hasa wanafunzi ambao baadhi yao hulalamika kushindwa kulipia au na kudai kutaka kurejeshewa fedha zao wakati huohuo wakiwa tayari wameshakamilisha mchakato wa uombaji na fedha hizo kupaswa kutumika kama ada ya uombaji.
Chanzo:Habari Vyuoni