Polisi nchini Ufilipino, wamesema kuwa wamewakamata
washukiwa wa uhalifu katika mitandao ambao ni sehemu ya kikundi cha watu
wanaowahadaa watu kwenye mitandao ya kijamii kote duniani.
Washukiwa hao huwashawishi watumiaji wa Internet au walengwa
wao katika nchi za kigeni kujipiga picha wakiwa uchi na wakiwa katika vitendo
vya mapenzi na kujirekodi kisha kuwatumia.
Wahalifu hao baadaye hudai kiasi Fulani cha pesa kutoka kwa
walengwa la sivyo huwatishia kuwa watawatumia jamaa wao picha na video hizo.
Polisi wamefanikiwa kuwakamata washukiwa 58 katika
operesheini hiyo iliyohusisha polisi wa kimataifa Interpol.
"Lengo la washukiwa hawa ni kutengeza akaunti kwenye
mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwatafuta wateja wao hasa wazee katika nchi
za kigeni,’’alisema afisa mmoja wa polisi.
"Katika akaunti zao hizo wao hujidai kuwa ni wasichana
wenye asili ya Asia wanaotafuta wapenzi katika nchi za kigeni.’’
"Baada ya kujuana vyema na watumiaji wa mitandao
wasiojua kuwa wanahadaiwa, wao huwakaribisha kuwa marafiki zao kwenye mitandao
, kuwasiliana nao kwa njia ya video kwenye mitandao hiyo hiyo na kisha kufanya
nao vitendo vya mapenzi kupitia kwa kompiuta huku wakirekodi kila
kinachofanyika. ‘’
Kanda hizo sasa hutumiwa kama njia ya kupata pesa kutoka kwa
waathiriwa kwa kutumia vitisho kuwa watasambaza kanda hizo kwa watu wa karibu
wa waathiriwa la sivyo walipwe kati ya dola 500 na 2,000. Pia hutishia
kusambaza kanda hizo kwenye mitandao ya kijamii.
Afisa mkuu wa Interpol amesema kuwa uhalifu huo umeenea sana
kwenye mitandao. Uhalifu wa aina hii hauna mipaka umeenea kote , sio Ufilipino
peke yake.
Chanzo:BBC-SWAHILI