Kwa mujibu wa maelezo ya Lucy Kinunda,
Mkurugenzi wa Masuala ya Malipo wa BoT kikosi kazi kinaundwa na BoT,
Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Chama cha Mabenki nchini (TBA) na Idara
ya Polisi ya Upelelezi wa Jinai inayoshughulikia vitengo vya
uhalifu wa fedha na wa mtandao.
Katika muendelezo huo Kinunda alisema BoT
imeziagiza benki zote kutoa mafunzo ya wafanyakazi ya kutunza siri na
taarifa za ndani za wenye akaunti ili kuzuia uhalifu dhidi ya amana
zao.
Pia BoT imeagiza wafanyakazi
wasiowaaminifu wanaoshirikiana na wahalifu kuadhibiwa kikamilifu pia
kufanya mchujo wa wafanyakazi kabla ya kuwaajiri.
Pia imewataka kuwahamasisha wateja kutunza
neno ama namba ya siri na kuacha kuzitoa kwa jamaa na ndugu zao, pia
wametakiwa kufuatilia usalama kwenye ATMs na kuanzisha mifumo ya
kurekodi matukio ya wanaotoa fedha kwenye mashine hizo na kuhimizwa
kuweka kamera za CCTV.
BoT imeyaagiza mabenki kupambana na kudhibiti wajanja wanaotumia mbinu za kuchota taarifa za wateja kwenye mashine hizo.
Baadhi ya mbinu zinazotumiwa ni kukamata
kadi , kuweka vifaa vya kunakili na kunasa namba ya siri na utambulisho
wao ili baadaye waweze kuandaa mbinu za kuiba kwa njia ya mtandao.
Kinunda alisema BoT imewashauri wenye
mabenki kutumia viwango vya kimataifa vya kuhakikisha usalama wa kadi za
ATMs za Visa na Master Card vya EMV.
EMV ni mikakati ya kimataifa ya
kuziwezesha kadi za Master Card na Visa kuwa na usalama na kuziepusha
zisitumiwe kihalifu na kuzilinda ili zibakie kuwa kadi zinazoweza
kuingilia kwenye ATM ya benki yoyote ya kimataifa
.
Pia Benki Kuu kwa mujibu wa Kinunda
itaendelea kupitia sheria za malipo ya kimtandao ili kudhibiti upungufu
na kujiimarisha zaidi ili kuepusha uhalifu unaoweza kutokana na
malipo ya mtandao.
Baadhi ya mbinu za wizi wa mtandao ni
kupachika kifaa kama film inayoweza kurekodi taarifa za mteja kuanzia
namba au neno la siri, kiasi cha fedha, jina na kumbukumbu zote.
Kikaratasi hicho huwekwa juu ya eneo
ambapo kadi ya ATM huingizwa. Mteja anapochomeka kadi film husoma
taarifa zake na kuzibakiza mikono mwa wezi ambao huzitumia kuchonga
kadi mpya na kumwibia licha ya kwamba ametunza kadi yake.
Lakini pia wafanyakazi wa mabenki wa
idara za teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) wanadaiwa
kushirikiana na wezi hao .
Pia zipo taarifa kuwa baadhi ya watumishi
wasio waaminifu wa kampuni zinazotengeneza kadi za ATM hushirikiana na
wezi wa mtandao kuandaa kadi mpya ili kufanikisha wizi wa ATMs.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI