Watu
wawili wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa wakiiba fedha kwa kutumia
kadi 30 kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM) ya Benki ya Afrika (Boa)
eneo la Sinza jijini Dar es Salaam. Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kadi hizo ni za
wateja mbalimbali wa benki ya Barclays na walitaka kuiba fedha hizo kwa
kutumia kadi hizo katika benki ya Boa.
Kamanda
Kenyela alisema watuhumiwa hao ambao walikamatwa jana saa 6:00 mchana,
wametambuliwa kuwa ni raia wa Msumbiji lakini hakuwataja majina yao.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaojihusisha na wizi wa namna hiyo.
Aidha, Kamanda Kenyela alisema wizi kama huo wa kutumia mashine na kadi
za benki, umekuwa ukitokea mara kwa mara jijini Dar es Salaam.
Alisema wengi wanaoibiwa fedha katika mashine za ATM, hawana uelewa wa
kutosha namna ya kuzitumia hivyo kuwalazimu kuomba msaada kwa jirani,
jambo linalowasababishia kuibiwa namba za siri na hatimaye kuibiwa.
Kamanda Kenyela aliongeza kuwa wizi mwingine ulitokea mwaka jana ambapo
watuhumiwa wawili raia wa kigeni walikamatwa wakiwa na ATM walizokuwa
wakizitumia kuibia fedha.
Mei 29 mwaka jana, Polisi jijini Dar es Salaam walimkamata raia mmoja wa
Bulgaria, ambaye alinusurika kuuawa na wananchi baada ya kudaiwa kuiba
dola za 23,000 za Marekani kwenye ATM.
Tukio hilo lilitokea katika benki ya Standard Chartered, tawi la Ilala jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo aliokolewa na askari waliokuwa doria.