Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy |
Kuzimwa
kwa mitambo ya kurushia matangazo ya televisheni kwa mfumo wa analojia,na kuwa katika mfumo mpya wa digitali kumesababisha sintofahamu ya wakazi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam kushindwa
kupata matangazo. Mitambo hiyo ilizimwa saa sita usiku Desemba 31 mwaka huu kwa maelekezo ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Sintofahamu hiyo imeonekana kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, kwa kutopata matangazo ya televisheni licha ya kununua ving’amuzi.
Aidha, wamesema chaneli tano zilizopewa leseni na serikali kuendelea kurusha matangazo yao, nazo zinaonyesha chenga chenga.
Baadhi ya watu wamekaririwa na vyombo vya habari wakidai kuwa mfumo huo umeleta usumbufu mkubwa kwao.
Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko yao, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa
TCRA, Innocent Mungy akizungumza na wanahabari amesema kuwa kinachowafanya wananchi washindwe kupata matangazo ni wao wenyewe
kushindwa kuunganisha ving’amuzi.
Mungy aliwataka wananchi kubadilika na kutumia mafundi wa kampuni zinazouza ving’amuzi badala ya wao wenyewe kujigeuza mafundi.
Alisema huduma ya kufungiwa king’amuzi inatolewa bure na hakuna
haja ya mtu kupanda juu ya nyumba yake na kuanza kufunga bila kujua
anachokifunga.
Kabla ya kuzimwa mitambo hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, akizungumza na
waandishi wa habari, alisema hata kama mitambo hiyo itazimwa, lakini
chaneli tano za hapa nchini zitaendelea kurusha matangazo yake kama
kawaida.
Ving'amuzi vyagombewa
Wakati zoezi la kuhamia dijitali likiendelea, blog hii ilishuhudia mamia ya wakazi wa
Jiji la Dar es Salaam walifurika katika maduka mbalimbali ya mawakala wa
kampuni ya Star Times kuendelea kununua ving’amuzi kwa ajili ya
televisheni zao.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi hao walikosoa huduma zilizokuwa zikitolewa
na mawakala hao kwa madai kwamba hazikidhi kiwango kinachotakiwa.
Utafiti uliofanywa na blog hii umegundua kuwa ving'amuzi sasa vinauzwa kuanzia sh 39,000 hadi sh 62,000 za kitanzania.
Afisa Masoko wa kampuni ya Star Times, Erick
Cyprian, alisema watu walinukuu vibaya kuhusiana na suala la punguzo la
manunuzi kwa kipindi cha kuelekea sikukuu.
“Punguzo la manunuzi ya king'amuzi halihusiani na muda wa hewani, hivyo
wengi wao wanadhani wakishanunua king'amuzi kwa bei ya Sh. 39,0000,
watapata muda wa maongezi moja kwa moja,” alisema Cyprian.
TCRA imekuwa ikieleza kuwa hatua ya kuhamia digital ni kufuatia Shirika la Kimataifa la Mawasiliano(ITU),kuzitaka nchi zote duniani kuhamia kwenye mfumo wa kurusha matangazo kwa njia hiyo ifikapo julai 2015.
Desemba 31,2012 Mamlaka hiyo inayosimamia mawasiliano nchini Tanzania ilieza kuwa mitambo ya analojia itazimwa katika mikoa ya Dar es salaam,Dodoma na Tanga ambapo zoezi hilo litahamia mkoa wa Mwanza na Machi 31,2013 itakuwa ni zamu ya mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na mkoa wa mwisho utakuwa ni Mbeya ambako watazima Aprili 30.
Kutokana na mfumo mpya wa digitali matangazo ya televisheni yanapatikana kupitia ving'amuzi ama madishi ya satalaiti.