Friday, January 25, 2013

MITAMBO YA ANALOJIA TANGA,DODOMA KUZIMWA JANUARI 30

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaendelea kutoa elimu kwa umma ikiwa ni maandalizi ya zoezi la uzimaji wa mitambo ya analojia kwa mikoani.
Januari 30, mwaka huu, itakuwa ni zamu ya mikoa ya Tanga na Dodoma.

Hii ni baada ya zoezi hilo kuanza na Kanda ya Dar es Salaam, Desemba 31, mwaka jana.

Mbali ya Dar es Salaam, maeneo mengine kulikozimwa mitambo ya analojia siiku hiyo ni katika miji ya Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe na Mkuranga mkoani Pwani.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano TCRA, Innocent Mungy, alisema tayari ratiba ya mikoa mingine itakayofuatia katika zoezi hilo, imeshatolewa kupitia vyombo vya mbalimbali vya habari. 

“Tarehe 30 tunatarajia kuzima mitambo ya analojia mkoa wa Dodoma na Tanga  na baada ya hapo Februari 28 , mwaka huu itakuwa zamu ya mkoa wa Mwanza, Machi 31 ni zamu ya Arusha na Moshi na Aprili 20 itakuwa ni kanda ya Mbeya. Tutaendelea na utaratibu huo ili kuhakikisha mpaka ifikapo Juni, 2015, tumekamilisha zoezi hilo kwa mikoa yote,” alisema Mungy.

Alisema licha ya changamoto ya uelewa mdogo wa watu juu ya matumizi ya ving’amuzi, bado mamlaka inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa jamii kupitia matangazo, vipindi katika redio na kufanya mikutano mbalimbali.

"Hivi sasa ninavyoongea nipo Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwa mkoa huu. Moja ya vitu tunavyo vifanya, ni utoaji wa elimu kwa wananchi," alisema.

"Tunawaelekeza wananchi kuhakikisha kwamba wanakuwa na uelewa  juu ya mfumo mpya wa dijitali pamoja na matumizi ya ving’amuzi," alisema.

Naye Afisa Mauzo wa kampuni ya Starmedia inayotoa  ving’amuzi vya Startimes,  David Kisaka, alisema kwa sasa kampuni hiyo imejipanga vizuri kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi katika matawi yake yote ikiwamo kuweka wafanyakazi katika idara kulingana na ujuzi.

Kisaka aliwaomba wananchi kufanya manunuzi ya ving’amuzi mapema kabla ya siku ya uzimaji wa mitambo kufika katika eneo husika, ili kuepuka usumbufu kama uliojitokeza jijini Dar es Salaam.

“Tumepata usumbufu mkubwa sana hapa Dar es Salaam sababu watu wengi walisubiri mpaka mitambo izimwe ndipo wanunue ving’amuzi.  Sasa nawaomba sana wananchi wa Tanga na Dodoma wanunue ving’amuzi hivi mapema ili hata kama kuna matatizo yoyote, tuwasaidie badala ya kusubiri mpaka siku ya uzimaji,” alisema.
 

CHANZO: NIPASHE

Popular Posts

Labels