Monday, June 30, 2014

FACEBOOK YALAUMIWA NA WATUMIAJI

 


Mtandao wa Facebook umelaumiwa kwa kuwafanyia wateja wake utafiti wa kisaikolojia bila ya kuwajulisha.

Nia ya utafiti huo ilikuwa kujua kama wateja wake wamebadili tabia ya kuweka picha na mawazo yao katika mtandao huo kutokana na kukasirishwa na tabia za baadhi ya watumiaji wenzao.
Utafiti huo uliohusisha takribani watumiaji 700,000 unaonyesha kuwa Facebook inacheza na taarifa za watumiaji wake ili kupata hisia zao katika kile wanachokiweka kwenye mtandao huo.

Hata hivyo mtandao wa Facebook umekanusha madai hayo na kwamba hakuna mtumiaji binafsi aliyelengwa na utafiti huo uliofanywa na mtandao huo kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Cornell na California.

“Ngoja tuuite utafiti kama Facebook wenyewe wanavyouita, lakini ni dalili za wazi za kushindwa kuzingatia maadili na nguvu ya kulinda haki za watumiaji wake” amesema Kate Crawford katika ukurasa wake wa Twitter.

Waziri wa kazi Jim Sheridan mjumbe wa bodi ya mawasiliano ameagiza uchunguzi kufanyikadhidi ya mtandao huo wa Facebook katika tuhuma hizi.

Hata hivyo Katherine Sledge Moore, Profesa wa Saikolojia katika chuo cha Elmhurst , Illinois amesema kwa jinsi ambavyo Facebook wamekuwa wakishughulika na taarifa za wateja wake makubaliano yaliyopo katika utafiti huo hadhani kama yapo nje ya hali ya kawaida.

Adam Kramer kutoka Facebook mmoja kati ya walioandaa taarifa ya utafiti huo anasema wanadhani kuwa ilikuwa mhimu kwao kutafiti mashaka yanayowakumba watumiaji hasa katika mawazo yanayowekwa na marafiki zao na jinsi yanavyowafanya wafikirie tofauti .
Chanzo:BBC

Saturday, June 21, 2014

TAHADHARI – UTAPELI KUPITIA CRDB INTERNET BANKING

Kuna Utapeli umeanza kusambaa saa chache zilizopita kupitia CRDB INTERNET BANKING .

Anayefanya utapeli huu ametengeneza majina bandia ya watu maarufu kama wanasiasa na wanamuziki kisha anaingiza watu kwenye orodha ya namba za mawasiliano alizohifadhi  halafu anawatumia ujumbe huu kama vile yeye ni mtu halisi .

Mtu anapokubali anampa huyu jamaa taarifa zake za benki halafu mwisho wa siku hela zake zinaweza kuhamishwa kwa njia ya mtandao .
MFANO WA UJUMBE NI HUU
-----------------------------------------------------
Habari za wakati ndugu watanzania! Kwa yoyote ambae amejiunga na huduma ya CRDB Bank kupitia Online. Internet Banking sio SIM BANKING alie jiunga na Internet Banking. Tafadhali naomba tuwasiliane kuna project maalum yenye faida kwangu nakwako pia kwa kushirikiana nao CRDB Bank. Malipo ni kila wiki katika hiyo project. Nitumie meseji inbox kama umejiunga na internet banking na unahitaji kushiriki katika hii project
==============================================================
Mpaka sasa hivi nimegundua majina 2 ya Kala Jeremia ambaye ni mwanamuziki na Jerry Silaa ambaye ni mwanasiasa .
Tuchukuwe tahadhari na tusambaze ujumbe huu .
Na:Yona Maro

Friday, June 20, 2014

VITAMBULISHO VYA KUPIGIA KURA TANZANIA KUTOLEWA KWA TEKNOLOJIA YA BIOMETRIC VOTER REGISTRATION



Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania Mh.Jaji Mstaafu Damian lubuva amesema tume hiyo  inatarajia kuboresha daftari la wapiga  kwa kutumia teknolojia mpya ya  “BIOMETRIC VOTER REGISTRATION” (BVR) ili kuwapatia watanzania vitambulisho vipya vya kupigia kura. 

Akizungumza wahariri wa vyombo vya habari katika ukumbi wa hoteli ya JB Belmonte jijini Dar es salaam juni 19 mwaka huu Lubuva  amesema tume ya uchaguzi  imeamua kufanya maboresho ya daftari la kudumu  la wapiga kura kwa kutumia teknolojia hii mpya ya biometric voter ili kwenda na wakati pia ni mfumo wa kuchukua na kupima taarifa  za mtu kibaiolojia au tabia ya mtu  na kuzihifadhi kwa ajili ya utambuzi ambapo alama za vidole  kumi, vya mikono, picha na saini  ndizo zitakazochukuliwa na kuhifadhiwa  kwenye kanzidata (database) ya wapiga kura.



Mh. Jaji pia amefafanua zaidi kwa kusema  “mfumo huu utasaidia sana kuwa na daftari  sahihi na linalotumika kwa ajili ya upigaji wa kura ya maoni  na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwa mfumo huu utatumika tu kwa ajili ya  kuandikisha wapiga kura na si kwa ajili ya upigaji kura za kielektroniki(e-voting) au vinginevyo”

Amesema Lubuva amesema  uamuzi  kutumia mfumo huu umetokana na changamoto  zilizojitokeza  katika matumizi ya teknolojia ya optical mark recognition (omr) kwamba omr ilisababnisha daftari la kudumu kuwa na kasoro hivyo kusababisha wadau wa uchaguzi  uhalali wake.

Waapiga kura wote waliojiandikisha awali na wale wapya watalazimika  kujiandikisha  upya ili kuchukuliwa taarifa  za kibaiolojia  kwa waliopo kwenye daftari hata hivyo mpiga kura atatumia kitambulisho atakachopatiwa na tume baada ya kuandikishwa katika mfumo huu tu na si vinginevyo.

Thursday, June 19, 2014

TCRA YAWAONYA WANAOWACHAFUA WATU KWENYE MITANDAO


Mamlaka ya mawasiliano nchini ,TCRA, imewaonya wale wote wanaotumia mitando kuchafua na kudhalilisha watu waache mara moja vinginevyo watakabiliwa na mkono wa sheria.

Onyo hilo limetolewa jana mjini Arusha na Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano nchini TCRA, Dkt, Raynold Mtungahema, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maswali ya wanahabari kuhusu kuenea kwa picha chafu zinazowadharirisha watu mbalimbali kwenye mitandao..

Mtungahema, amesema matumizi ya mitandao ambayo sio sahihi ni kosa la jinai na hivyo wale wote wenye tabia hiyo waache mara moja na akawataka  wanaochafuliwa kupitia mitandao wafungue majalada polisi na mamlaka hiyo itasaidia kuwafuatilia wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria .

Alisema mitandao yote imesajiliwa hata kama aliyehusika kuchafua anaishi uvunguni atakamatwa kwa kuwa mitandao haipo kwa ajili ya matumizi yasiyo sahihi  ambayo hayaruhusiwi.

Mtungahema,  amesema  atakaebainika anatumia mtandao kumchafua mtu mwingine huyo amefanya kosa la jinai hivyo afikishwe mbele ya vyombo vya sheria kwa kuwa tayari zipo sheria zinazotoa adhabu kwa mtuhumiwa atakaepatikana na hatia.

Aliongeza kuwa TCRA, imeshapokea malalamiko mengi na tayari wahusika wameshatiwa mbaloni  na ufuatiliaji utaendelea ili mradi tu mamlaka hiyo itaarifiwe .

 

 

Nchi wanachama wa jumuia  afrika mashariki zimeaanza kikao cha siku nne  mjini Arusaha kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa chang moto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mawasiliano.

 

Mwenyekiti wa jumuia hiyo ya sekta za mawasiliano, EACO, Dakta   Fracis Wangusi, amesema sekta ya mawasiliano inakabilwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa haraka.

Wangusi ambae pia ni mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya,amezitaja sekta hizo kuwa ni pamoja na kuhama kutoka mtandao wa analojia kwenda digital na  matumizi ya visumbusi kwa ajili ya luninga.

Aliongeza kuwa , sekta ya simu inakabiliwa na changamoto ya kuwepo gharama kubwa za matumizi ya simu, usambazaji barua na vifurushi kunakofanywa namashirika ya posta unaotokana na ukuaji wa mji ambao haujapangiliwa ,matumizi ya  vikwazo vya kuchelewesha huduma ya haraka ya internet .

 

Alisisitiza kuwa ili kupatikana kwa mafanikio hayo ni kuondoa vikwazo na kuhimiza uwekezaji kwenye sekta ya mawasiliano ICT.

TEKNOLOJIA YA KUKABILIANA NA MADAWA YA KULEVYA YAONESHA MAFANIKIO UWANJA WA NDEGE WA JULIUS NYERERE



Waziri na waziri wa uchukuzi Dr Harrison mwakyembe  amesema kuwa Teknolojia ya kisasa inayotumika katika  uwanja wa ndege wa  kimataifa wa Julius Nyerere kukabiliana na dawa za kulevya imeonesha mafanikio  katika kuwabaini wanaojihusisha na usafirishaji  wa dawa hizo.


Dr Mwakyembe  ameyasema hayo  wakati akifungua  semina ya baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya  Tanzania  iliyofanyika  jana jijini Dar es salaam.


Mwakyembe amesema wanatumia teknolojia  ya kisasa katika uwanja huo ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa  kupunguza  aibu ya watu  wanaokamatwa  na dawa za kulevya  katika nchi mbalimbali duniani  wakitokea Tanzania .


Taarifa zinaonesha kuwa  kwa kipindi cha kati ya ya januari  2013  na mei mwaka huu   jumla  ya kilogramu 85,840  za bangi  na kilogramu 18,202  za mirungi zilikamatwa.


Dr Mwakyembe ameyataja madawa mengine kuwa ni heroini kilogramu 1,547 , kokeini kilogramu 15.4  na kwamba watuhumiwa wakifikishwa katika vyombo vya sheria
.

Dr Mwakyembe ameongeza kuwa wizara yake ipo katika mchakato wa kutafuta kampuni yenye teknolojia ya kisasa zaidi itakayoimarisha ulinzi na kukabiliana na hila zote za wasafirishaji na kuomba  ushirikiano wa vyombo vya ulinzi  na usalama kubaini mtandao wa biashara hiyo ili kupambana na wimbi la usafirishaji wa dawa za kulevya dunia.


Tuesday, June 17, 2014

SIMU YA MKONONI YAATHIRI MBEGU ZA KIUME

 

Tathmini ya utafiti kutoka chuo kikuu cha Exeter nchini Uingereza, inaonyesha kuwa kiwango cha mbegu za uzazi za wanaume huathiriwa kwa kuweka simu za mkononi kwenye mifuko ya suruali.

Hata hivyo ,mwanasayansi wa maswala ya uzazi na shahawa,anasema kuwa ushahidi huo bado hauna uhakika wowote hivyo basi simu yake bado inaendelea kukaa mfukoni mwake.
Uchunguzi huo uliochapishwa katika jarida la 'Environment International' ulilaumu mnunurisho wa kielectromagnetiki kuwa chanzo kikuu kinachoathiri mbegu za wanaume.

Wataalamu walichanganua utafiti tofauti kuonyesha ubora wa shahawa wakihusisha wanaume 1,492.

Hii ilijumuisha kupimwa kwa shahawa zilizowekwa wazi kwa mnunurisho wa simu za rununu, kwa maabara na udadisi wa wanaume katika kliniki za uzazi.

Kiongozi wa uchunguzi huo Dkt.Fiona Mathews aliambia BBC kuwa kutokana na uchunguzi huo,mmoja tu ndio ulionyesha uhusiano kati ya utumizi wa simu na kudidimia kwa ubora wa shahawa.

"Nafikiri kwa mwanamume wa makamu hakuna haja ya kuingiwa na hofu,iwapo unajua una uwezekano wa kuwa na shida ya kizazi basi itakuwa jambo la busara kutoweka simu mfukoni ,pia kugeuza mtindo wako wa kula."

Mbegu za uzazi za wanaume zinasemekana kuathirika kutokana na simu za mkononi

Alikubali kukosolewa na wanasayansi wengine huku akiunga mkono kuwa kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi zaidi.

Dkt,Mathews alimaliza kwa kusema"hili ni jambo la kusisimua lakini hatusemi kwa uhakika kuwa kila anayebeba simu mfukoni atakuwa na shida ya kizazi."

Dkt.Allan Pacey kutoka chuo kikuu cha Sheffield anasema kuwa wazo hilo la kudidimia kwa shahawa na kuharibu "DNA" linatokana na mnunurisho wa kielectromagnetiki zinazopatikana kwenye simu na pengine joto aidha moja kwa moja kutoka kwenye simu au mnunurisho.
Dkt huyo anayefanya uchunguzi wa shahawa bado hajashawishika akisema ushahidi huo hauna msingi na ataendelea kuweka simu mfukoni.

Aliambia BBC,"kumekuwa na shauku kwa mda kama kuweka rununu mfukoni kunaweza changia kudidimia kwa ubora wa shahawa na nguvu za kiume kivyovyote.

"Kumekuwa na habari zisizokuwa na msingi lakini kwa maoni yangu uchunguzi uliofanywa hadi kufika sasa haujakuwa wa kutosha kwa sababu wachunguzi aidha hawakuhifadhi shahawa vile inavyofaa ama wamedadisi matumizi ya simu kati ya wanaume bila kuzingatia mambo mengine kama mitindo yao ya maisha.

"Tunayohitaji ni uchunguzi kufanywa ambapo utumizi wa simu unazingatiwa vile vile tabia zinazoathiri maisha yao.
Hadi pale tutakapo tafakari hayo,nitaendelea kuweka simu yangu katika mfuko wa mkono wa kulia wa suruali yangu!"
Chanzo:BBC


Saturday, June 14, 2014

GOOGLE YATUMIA MOZILLA FIREFOX KUTANGAZA MECHI ZA KOMBE LA DUNIA


Toka kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia la mchezo wa kandanda huko nchini Brazil juni 12,mwaka huu Google kupitia kivinjari chake cha Mozilla Firefox wamekuwa wakiweka matangazo ya mchezo unaotarajiwa kuchezwa.

Utaratibu huo umekuwa ukibadilika kwa kila mechi inayofanyika, pichani ni picha iliyokuwepo wakati wa mchezo baina ya Uingereza na Italia ambao unaonesha rangi nyeupe iliyotumiwa katika jezi za wachezaji wa Uingereza na Bluu kwa wachezaji wa Italia.

Wednesday, June 11, 2014

KENYA KUANZISHA KITENGO MAALUM CHA KUPAMBANA NA UHALIFU MTANDAO

Bwana. Keriako Tobiko
 
Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma ya nchini Kenya Bwana. Keriako Tobiko ametangaza kuanzishwa kwa kitengo maalumu kitakacho pambana na  uhalifu mtandao katika ofisi yake. Amedai hatua hii imefikiwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya uhalifu unaofanywa na wahalifu wenye uelewa wa teknolojia.

"Kwa mtazamo wa kuongezeka kwa uhalifu wa mtandao, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Umma (ODPP) imeanzisha kitengo maalumu kusimamia mashtaka ya wahalifu wa mtandao," Tobiko alisema, kwa mujibu wa The Standard la Kenya.

Takwimu zinaonyesha Kenya inapoteza kiasi cha shilingi bilioni 2 (Dola milioni 23.3) kwa mwaka kupitia uhalifu wa mtandao." Aliongeza Bwana Tobiko.

Hata hivyo, alisema, jitihada za kuwakamata na kuwashitaki watuhumiwa zimekua ngumu kutokana na ukosefu wa sheria zinazofaa, zikiwaacha huru wahalifu kufanya uhalifu wa mtandao ambao unatishia usalama wa taifa, miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na haki ya usiri wa raia.

"Kwa kutambua kwamba kwa sasa kuna sheria zisizotosheleza za kushtaki uhalifu wa mtandao, ODPP imeandaa warsha ya kupitia upya sheria zilizopo na kuandaa rasimu ya mswada wa kina kuhusu uhalifu wa mtandao kulingana na taratibu husika za kimataifa zinazofaa," Tobiko alisema, akiongeza kwamba matumaini ya kuwa na mswada wa kina wa uhalifu wa mtandao yatakamilika mwaka huu.

Saturday, June 7, 2014

WAHALIFU MTANDAO WAITIKISA KOLOMBIA


Polisi Wa  kuzuia uhalifu Mtandao.
Wakala unaofuatilia matumizi ya mitandao duniani (IAB) umebaini watumiaji wa intaneti nchini Kolombia wamefikia asilimia 70 ya wakazi milioni 47 wa nchi hiyo huku ikibainishwa ya kuwa nchi hiyo ukuaji wa uhalifu mtandao umeendelea kukua kwa zaidi.

Mwaka 2011 Kolombia ilikua Nchi ya kwanza kuanzisha sera ya usalama mitandao katika ukanda wan chi za latini amerika kupitia baraza la taifa la nchini humo linaloshughulikia maswala ya sera za uchumi na kijamii (COMPES).



Kupitia Sera hiyo, Paliundwa kikundi kinachoshughulikia maswala ya mitandao kilicho unganishwa moja kwa moja na wizara ya ulinzi pamoja na polisi wa nchini humo kupitia kitengo kinachojiusisha na maswala ya ulinzi mtandao.
Pamoja Na jitada zote hizo bado nchi hiyo imeendelea kukumbwa na mamia ya uhalifu mtandao unaofanywa dhidi ya raia wake na serikali ya nchi hiyo na ndipo palipo anzishwa misheni inayotoa misaada ya kiufundi ya usalama mitandao jijini Bogota nchini humo.
Kolombia waliunganisha nguvu na wataalam kutoka nchi nyingine  kuanzia tarehe 31 ya mwezi machi hadi tarehe 4 ya mwezi aprili mwaka huu (2014) ili kupitia na kuchambua  hali ya usalama mitandao ya nchi yake na kutoa mapendekezo stahiki.

Bwana Belisario Contreras kutokea  (CICTE) alieleza ushauri na mapendekez yaliyo tolewa yataingizwa katika vitendo ili kukabiliana na asakata la uhalifu mtandao nchini humo.

Aidha, Erwin Doutzauer strampfer kutokea chuo kikuu cha Oxford alipokua akichangia hali ya uhalifu mtandao amenukuliwa akisema kutokana na uhaba mkubwa wa wataalam wa maswala ya ulinzi mtandao shabaya ni kuendelea kukuza nguvu watu na kusisitiza changamoto kubwa iliyoko sasa ni kuingiza mafunzo ya usalama mitandao kuanzia ngazi ya chini mashuleni ili kuwezesha vijana wadogo kujua jinsi ya kujilinda mitandaoni ambapo ameeleza kumekua na kesi za watoto kujiua kutokana na kile alicho kisema kama “Cyberbulling”.

Ufafanuzi wa hili kwa lugha ya kingereza unasomeka "HAPA" na taarifa ya awali ya kingereza  iliyo ainisha juhudi za nchi hiyo dhidi ya mapambano ya uhalifu mtandao pia inapatikana "HAPA" .

Na:Yusuph Kileo

TUJIFUNZE KUTOKANA NA CHINA KUKATAZA WINDOWS 8

Katika wiki chache zilizopita kulikuwa na msuguano kati ya serikali ya Marekani na China , Serikali ya Marekani inailaumu china kwa kufanya udukuzi kwenye kampuni zake na biashara nyingine huku china nayo ikiilaumu marekani na mwishowe ikaamua kukataza matumizi ya windows 8 kwenye kompyuta zote za serikali na taasisi zote zinazopewa fedha na serikali ya nchi hiyo .

Serikali ya China na wataalamu wake kadhaa wanasema matumizi ya windows 8 ni hatari kwa usalama wao na ustawi wao , kwahiyo wamekataza na kuendelea kutengeneza program yao ya COS China Operating System kwa ajili ya matumizi ya serikali pamoja na taasisi zake .

Kwan nchi za ulaya suala kama hili liliwahi kutokea miaka kadhaa iliyopita , lakini umoja wa ulaya ulienda mahakamani na mahakama ikaamua Microsoft itoe source code kwa umoja wa ulaya ili waweze kubadilisha na kuweka mambo yao kwa maslahi ya umoja wa ulaya .

Kitu kikubwa ambacho serikali ya uchina inalalamikia kuhusu Windows 8 ni hii source code , serikali ya china inataka source code ya bidhaa hii ili iweze kuifanyia mabadiliko iendane na maslahi yake haswa kwenye mambo ya ulinzi na usalama .

Hapa nchini kwetu tumeona taasisi mbalimbali na wizara mbalimbali za serikali tena nyeti zikitumia bidhaa mbalimbali za windows bila kufanya mabadiliko yoyote kwa ajili ya usalama wao , tumeona watu haswa viongozi wakinunua kompyuta na vifaa vingine vya mawasilino na kuvitumia kuhifadhi taarifa nyeti bila vifaa hivi kuchunguzwa au kubadilishwa chochote .

Suala la serikali ya China lituamshe na tuanze harakati za kuangalia maslahi makubwa ya taifa wakati wa manunuzi na matumizi ya vifaa na program mbalimbali toka nchi za nje , program hizi na vifaa vyake vinaweza kutumika kwa urahisi kuhamisha taarifa na chochote kile au kufanya uhalifu bila mnunuzi au mtumiaji kujua .

Wakati serikali inafikiria kupeleka muswada wa sheria ya usalama wa mtandao bungeni , ni vizuri suala kama hili lijulikana na wataalamu watakaojadili sera au chochote kinachohusiana na usalama wa Taifa .

Huwezi kulinda taifa kama taarifa zako zinaweza kuchukuliwa au kuangaliwa na mtu akiwa popote duniani .

YONA F MARO 
0786 806028

TIGO,AIRTEL,ZANTEL WAUNGANISHA HUDUMA ZA MIAMALA YA KIFEDHA KATIKA SIMU ZA MKONONI

Kampuni za Simu za mkononi za Tigo,Airtel na Zantel zimeunganisha huduma zao za kutoa,kutuma na kuweka fedha na sasa mteja anaweza kutuma fedha kutoka mtandao mmoja kupitia mwingine.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa hivi karibuni na kampuni hizo imesema kuwa wote wanaotumia huduma hiyo wataweza kutumiana fedha kupitia simu zao za mikononi pasi na tatizo baada ya kampuni hizo kuunganisha huduma zao.

Huduma hiyo inayotajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu itawafanya wateja wa mitandao hiyo kutumiana na kupokea fedha moja kwa moja kwenye akaunti zao tofauti na ilivyokuwa awali.

Matumizi ya simu za mkononi kufanya miamala ya kifedha yamezidi kukua kwa kasi nchini Tanzania,kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makambe Mbarawa hadi sasa kuna watumiaji wa huduma za kifedha kwa simu za mkononi 12,330,962




Thursday, June 5, 2014

TANZANIA:MITAMBO YA KUBAINI ULAGHAI KWENYE SIMU YAWEKWA

Serikali ya Tanzania imeweka mitambo ya aina tatu kukabili ulaghai na udanganyifu kwenye mawasiliano na miamala ya simu za mkononi.

Taarifa hiyo imetolewa hivi karibuni bungeni na Naibu Waziri wa Mawasiliano nchini Tanzania,Sayansi na Teknolojia,January Makamba.Amesema tayari watu watu watatu wamekamatwa kwa kutaka kuiibia serikali shilingi bilioni nane.

Makamba amesema upo mtambo wa kutambua kila kifaa kama vile simu,Ipad au komputa iliyotumika katika matukio ya kihalifu kwa kuizima na kufahamu umbali au eneo kilipo kifaa husika kinachotumika kutuma ujumbe wa matusi,Ulaghai au wizi wa fedha za wateja.

Waziri huyo amefafanua kuwa serikali imeanza kubana kampuni za simu kuhakikisha zinatoa huduma bora za usikivu wa simu,kushughulikia malalamiko ya wateja,kuhakikisha hakuna wizi wa fedha za wateja unaofanyika katika simu.

Wednesday, June 4, 2014

MAWASILIANO YA UJUMBE MFUPI WA SIMU YAZUIWA AFRIKA YA KATI


 


Maafisa wa utawala katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamebana matumizi ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi baada ya kusema kuwa ni tisho kwa usalama wa nchi.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano serikali.
Watumiaji wa simu za mkononi ambao wamekuwa wakijaribu kutuma ujumbe mfupi wanapata jibu hili: ''Ujumbe wako hauwezi kutumwa.''

'Wenye simu za mkononi hawaruhusiwi kutuma ujumbe mfupi kuanzia Jumatatu 2 Juni 2014 hadi itakapotolewa taarifa zaidi kuhusu agizo hili,'' huu ndio ulikuwa ujumbe wa wizara ya mawasiliano kwa kampuni za kutoa huduma za simu.

Inaarifiwa kuwa uamuzi huo ulifikiwa na waziri mkuu Andre Nzapayeke.

Tangu wiki iliyopita, kumekuwa na ghasia zaidi mjini Bangui, pamoja na kutolewa wito wa maandamano uliotumwa kwa simu kama ujumbe mfupi siku chache zilizopita.
 
Duru zinasema kuwa hatua ya kubana ujumbe mfupi wa simu itadumu kwa siku kadhaa kabla ya agizo lengine kubatilisha amri hiyo.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inakumbwa na vita kati ya jamii za wakristo na waisilamu imekuwa ikikumbwa na hali ngumu ya usalama pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya jamii hizo
Chanzo:BBC

UHALISIA WA TAKWIMU ZA MTANDAO WA INTANETI


Click the image to open the interactive version (via http://pennystocks.la).

Popular Posts

Labels