Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi
wa jumla wa kero kwa wateja wa huduma mbalimbali na bidhaa hapa nchini
kupitia mchakato unaoendelea kupitia mitandao ya kijamii ya Twitter na
Facebook.
Nafasi ya pili ilishikiliwa na Kampuni ya mawasiliano ya Tigo
na ya tatu kuchukuliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom.
Katika mzunguko wa kwanza jumla ya makampuni 29 yaliingia katika
kinyanganyiro na kufanikiwa kuchukua ushindi katika makundi mbalimbali .
Katika kundi la huduma za usafiri wa Anga , Shirika la Ndege la
Precision ndio liliongoza kwa kero na huduma zisizo na uhakika huku
kundi la huduma za maji likishikiliwa na Dawasco.
Kwa upande wa usafiri wa mabasi Kampuni ya Happy Nation iliongoza kwa
malalamiko kutoka kwa wateja huku kundi la ving’amuzi vya Televisheni
likiongozwa na Star Times.
Kwa upande wa huduma za maegesho ya magari , eneo la Magogoni Ferry
limelalamikiwa na wateja kwa huduma mbovu na kufanikiwa kushika nafasi
za juu katika kundi hilo.
Kwa upande wa wateja wanaolipia huduma za Televisheni kituo cha TBC
pekee ndicho kimelalamikiwa kwa kutokuwa na huduma za uhakika kwa
watazamaji wake.
Katika kundi la huduma za mawasiliano ya simu za mkononi , Kampuni ya
Tigo ndiyo iliibuka mshindi ikifuatiwa na Kampuni ya Vodacom.
Zoezi hili la kukusanya kero linafanywa na Wananchi kupitia akaunti
ya Twitter inayopatikana kupitia @hudumambayatz na facebook group
iliyopewa jina la HUDUMA BONGO ambapo huduma na bidhaa zote zinazolipiwa
na wateja mfano Burudani, Elimu, Hospitali, Hoteli, n.k zinazowakera
wateja zitaingia katika kinyanganyiro hicho.
Washauri wa kibiashara wa Huduma Bongo wanatoa wito kwa
viongozi wa juu wa Mashirika yote 29 yaliyotajwa kuchukua hatua
madhubuti za kuhakikisha wateja wao wanapata huduma bora kulingana na
fedha wanazotoa ili kuweza kuleta maendeleo ya Taifa.
Zoezi hili linaendelea ambapo katika mzunguko wa kwanza jumla ya kero
119 ziliwasilishwa na wateja endapo msomaji una kero iliyoshindwa
kupatiwa ufumbuzi na watoa huduma hawa unahitajika kuwa na akaunti
inayotambulika ya Twitter au Facebook na kujiunga na Huduma Bongo kisha
ueleze kero yako. Ukweli na Haki kuzingatiwa
Chanzo:wavuti.com