skip to main |
skip to sidebar
KAMPENI YA KUHAMASISHA MATUMIZI MAZURI YA MAWASILIANO
Siku za hivi karibuni, ongezeko la huduma za mawasiliano nchini
limekuwa kwa kasi sana. Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi
kifupi zimekuwa sana na kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Kutoka laini
za simu za mkononi milioni tatu tu mwaka 2000 hadi kufikia laini
28,000,000.
Watanzania walio wengi hivi sasa wanafaidika kwa
huduma za mawasiliano, yakiwemo mawasiliano ya simu za mikononi,
utangazaji. Vile vile huduma za ziada kama kutuma na kupokea fedha kwa
kutumia mitandao na simu za mkononi zimeongezeka maradufu. Wananchi
wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao, wanawasiliana kwa
kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na kadhalika.
Hali
kadhalika kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa watanzania
walio wengi kutoka watumiaji laki tatu miaka mitatu iliyopita hadi
watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni. Wengi wa watumiaji
wa intaneti matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na
matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, BBM,
LinkedIn na blog mbalimbali zinazotoa habari mbalimbali zikiwemo za
kimaendeleo, burudani pamoja na michezo.
Matumizi haya ya
intaneti yamewanufaisha watanzaia walio wengi kwani ni fursa murua ya
kujifunza kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari mpya,
kujifunza na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani
miongoni mwa watanzania.
Hata hivyo pamoja na maendeleo haya,
kumekuwepo na baadhi ya watu wachache wanaotumia mawasiliano ya simu,
mitandao ya kijamii, redio, TV na mawasiliano mengine kwa lengo la
kuvuruga amani, kuchocheo vurugu, kuchonganisha watu, kusababisha
ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na ukweli, kupotosha jamii na
hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
Julai 31,2013 Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) inazindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu
matumizi mazuri ya mawasiliano na inawatahadharisha wananchi kwamba
kutumia mawasiliano vibaya kama ilivyoainishwa katika sheria ya
Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 ni makosa.
Katika kampeni hii, Mamlaka inakusudia kuwasihi wananchi kuhakikisha
wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani, mshikamano na upendo
miongoni mwa watanzania.
Katika uzinduzi huu, Mamlaka
imewaalika baadhi ya watumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii ambao
wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watanzania walio wengi wanafaidika
na mawasiliano. Miongoni mwao wako wamiliki wa blog mbalimbali,
wasimamizi wa makundi mbalimbali katika mtandao wa FB na mengineyo. Nia
ya Mamlaka ni kuomba ushirikiano kwao ili waweze kushiriki katika
kampeni hii na kuwahamasisha mashabiki wao kutumia vizuri mitandao ya
kijamii ili kunufaisha Taifa letu kwa matumizi mazuri.
Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wote wanashauriwa kuunga mkono
juhudi zinazofanyika ili kufanikisha kampeni hii kwa ajili ya kudumisha
na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta ya
Mawasiliano inaendelea kuchangia uchumi wa Taifa na kuiweka Tanzania
katika mazingira mazuri zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Tunawasihi wananchi na watumiaji wa huduma za mawasiliano kuwa wakipokea
ujumbe wowote wa kueneza chuki, unaopelekea kuvuruga amani, uchochezi
na kuvuruga amani, toa taarifa kwa vyombo husika, kisha futa ujumbe huo.
Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa sehemu ya uhalifu.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
31 Julai 2013