Idadi ya watu wanaotumia huduma ya mtandao wa Intaneti nchini Tanzania imeongezeka kutoka watu 26,000 mwaka 2000 hadi kufikia watu milioni 5.9 Juni mwaka jana.
Ofisa wa Idara ya Maendeleo ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Teknohama) wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA) Connie Francis amesema hayo
wakati wa semina ya wadau wa mtandao wa Intaneti iliyohusisha uundaji wa
kamati ya mpito ya uanzishwaji wa Kituo cha ‘Mbeya Internet Exchange
Point’.
Amesema kutokana na umuhimu wa huduma ya intaneti
kwa shughuli mbalimbali, idadi ya watumiaji wa huduma hiyo nchini
imeongezeka kutoka watu 26,000 mwaka 2000 hadi kufikia watu milioni 5.9
mwaka jana.
Alisema huduma hiyo imerahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kibiashara, kiuchumi na kijamii.
Francis amesema kuwa baada ya kuonekana umuhimu wa
huduma hiyo TCRA imeamua kuanzisha mradi ambao utamsaidia mtumiaji
kupata huduma hiyo kwa ubora, urahisi na haraka zaidi na kwa gharama
nafuu.
Amesema katika kituo hicho watoa huduma wataweza
kuweka vifaa vyao na kupata fursa ya kuungana na kurahisisha maendeleo
ya mtandao wa Intaneti na kwamba itaisaidia nchi kudhibiti mawasiliano
ya ndani na kubaki ndani ya nchi badala ya kutoka nje ya nchi na kurudi
ndani.
“Mfumo uliopo kwa sasa ni pale mtumiaji wa mtandao
wa Intaneti mawasiliano yake kwenda nje ya nchi ya Tanzania na kurudi
hapa kwetu na ndipo baadae kuja kumfikia mhusika. Ni mfumo unaochukua
muda mrefu na gharama kubwa kutokana na mzunguko uliopo’’ amesema.
Tayari kamati ya mpito ya uanzishwaji wa kituo
hicho imeundwa ambapo imeshirikisha wadau wa mtandao wa Intaneti na
itakabidhiwa ofisi pamoja na vifaa hivyo kwa ajili ya kuanza kazi ya kusimamia mfumo huo mpya na kuhamasisha watoa
huduma ya mtandao wa Intaneti kujiunga na kituo hicho kwa ajili ya
kufanya kazi kwa ufanisi.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi