Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) kupitia Mkurugenzi wake Mkuu Profesa John Nkoma imesema namba za simu zilizosajiliwa nchini humo ni asilimia 93 na asilimia 7 hazijasajiliwa na kwamba asilimia iliyobaki inatakiwa kuondoka.
Akizungumza na wadau wa mawasiliano jijini Dar es salaam jana Mkurungenzi huyo amesema kuwa namba za simu lazima zisajiliwe kwa mujibu wa sheria ya Mawasiliano ya Elekroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010.
Amesema kisheria mtu anayetumia simu isiyosajiliwa akikamatwa anaweza kutozwa faini ya shilingi 50,000 za kitanzania ama kwenda jela miezi sita.
Katika vikao vya pamoja vilivyofanyika Aprili 4 na Aprili 11 mwaka huu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na kampuni zinazotoa huduma za simu za mkononi,zimekubaliana kuchukua hatua za kumaliza tatizo la usajili wa namba za simu na utaratibu wa kufungia namba zote ambazo hazikusajiliwa.
Profesa Nkoma amesema kuwa kwa kushirikiana na kampuni za simu na vyombo vya usalama imeanza kampeni endelevu ili kuwabaini wanaohusika na uvunjifu wa sheria kwa lengo la kuwalinda watumiaji wema.