Wednesday, April 24, 2013

TUWE MAKINI NA MATUMIZI YA MITANDAO JAMII


 
 

Mitandao ya kijamii ni mingi sana,ingawa facebook umekuwa maarufu pengine kuliko hata baadhi ya vituo vya redio ama televisheni.
Kwa sasa maelfu ya watanzania zaidi vijana wamejiunga na wanafurahia mawasiliano haya ambayo yameufanya ulimwengu kuwa kweli kijiji.

Ni kawaida sasa kujua anachofanya ndugu yako anayeishi Uingereza,Korea au Marekani ambako tumepishana kwa saa nyingi.Swali la msingi ni kuwa pamoja na raha hii inayotuweka karibu,unaitumia facebook kwa usalama na kwa manufaa?


Unadhani taarifa zako ulizoziweka hazina athari kwako?Tafakari kwa makini,iwapo hisia unazozitoa mara kwa mara zinachukuliwa na hata kueleweka kwa watu wengine,hapana shaka siku hizi facebook imekuwa kama kimbilio au beseni la kuzimwaga hisia za moyoni.

Utamkuta mtu anaandika kwa mfano "Nipo Zanzibar Francoroso hotel na my love'Unadhani ni sawa kila mtu kujua ratiba zako na mpenzi wako?Kuna manufaa yapi kwa umma na marafiki zako wote kujua ulipo na upo na nani?Unadhani marafiki zako hao pengine 300 wanakuwazia mema?
Wengine hutuma picha wakiwa nusu uchi na wanaposifiwa na marafiki zao kuwa wamependeza huona fahari na kumbe wanajidhihaki.

Mtandao huu ni mzuri endapo utatumiwa vyema,lakini napata shaka kuwa watumiaji wake wamejisahau kiasi cha kuyaweka maisha yao yote katika facebook.
Wapo wengi wanaofikia hatua ya kutoa siri zao ambazo ni vigumu kuzisema wazi hata mbele ya marafiki zao.
Ubora wa facebook ni mkubwa lakini pasipo umakini,yapo pia madhara makubwa.

Fumanizi nyingi zimetokea kupitia mitandao hii,talaka,mauaji na hata utekaji vimeshawahi kutokea kupitia facebook,Upo uhusiano uliovunjika tu baada ya mpenzi kubadilisha hadhi yake kutoka ya kuwa na mwenza kwenda single.Uelewa mdogo kuhusu ubinafsi au usiri wa taarifa zetu ndicho chanzo cha kujianika kiasi hiki katika mitandao hii.

Katika maisha haya ya leo,ambayo ni vigumu binadamu kuwajua adui zake ni vyema tukawa makini,wapo ambao huweka taarifa zao zote kuanzia tarehe ya kuzaliwa mwaka na mwezi,hii ni hatari kwani ni rahisi kwa watu wenye nia mbaya kukufanyia lolote au kutumia taarifa zako hata kukuibia.

Kuna kitu kingine nadhani watu hawafahamu kama kina madhara.Matukio na sehemu ulizotembelea kwa kipindi fulani kuonekana kwenye facebook katika eneo la tukio na mahali,Akaunti yako itaonesha mwezi uliopita ulitembelea maeneo na mambo kama hayo.

Inasikitisha kuwa mitazamo mingi ya watu imebadilika kutokana na matumizi ya facebook.Kwa kifupi,watu wanashindwa kujidhibiti.Ni rahisi kufuatilia mawasiliano kati ya watu wawili katika facebook na kujua iwapo kuna uhusiano wowote.

Utafiti mpya umebaini kuwa kati ya watumiaji 300 wa facebook,asiliamia19 hufuatilia tabia za wenza wao.Katika utafiti mwingine ilibainika kuwa watumiaji 1,000,asilimia 25 walivunja uhusiano kwa sababu ya facebook

Wapo wafanyakazi katika taasisi za dini waliojifanya watakatifu,wakatumia facebook kutuma picha wakinywa pombe wakafukuzwa kazi,wengine walimu halafu wanatuma picha wakiwa wanakunywa pombe au wamekumbatiana na wenza,hii inaharibu heshima kwa wanafunzi wako.Mitandao yote ya kijamii ina mengi mema,lakini tuwe makini na namna tunavyoitumia isitiathiri.
Na Florence Majani

Popular Posts

Labels