Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Zitto Kabwe hakuwa tayari
kueleza maeneo ambayo Serikali imekuwa ikipunjwa kodi na kampuni hizo na
badala yake amesema wameunda kamati ndogo ya watu watatu kwa ajili ya
kuchunguza wizi huo.
Kamati hiyo ilibaini madudu hayo baada ya kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).
Akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema wameitaka TRA kuandika mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho ya sheria ya fedha ya 2012, ili iwe na uwezo wa kuhakiki uwekezaji wa kampuni za simu na kufanya ukaguzi wa miradi husika ili kubaini kama inafanana na kodi inayotozwa.
Alisema kampuni hizo zina misamaha mikubwa ya kodi ambayo inatolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) bila kushirikisha wadau mbalimbali na kwamba hivi sasa Serikali inapata Sh300 bilioni tu kwa mwaka kama fedha za mapato ya kampuni hizo.
“Misamaha kwa kampuni za mawasiliano ni miaka mitano na TIC inaweza kuongeza miaka mingine mitatu. Kutokana na hali hiyo tunahitaji marekebisho ya sheria ili tuweze kuzibana hizi kampuni ziweze kulipa kodi na kuchangia pato la ndani,” alisema Zitto.
Zitto alisema mbali na mapendekezo hayo, pia wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua misamaha yote ya kodi inayotolewa na TIC ili kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi wa kuendelea nayo ama vinginevyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema: “Kuna fedha zinakatwa kienyeji tu na kampuni hizi, mfano kwa watu 5 milioni kwa siku wanapata Sh1.8 bilioni, sasa kama kampuni hii itakuwa na wateja zaidi inapata kiasi gani, fedha hizi hazipo katika mlolongo wa ukatwaji wa kodi.
“Pia tutahitaji maelezo ya jinsi mnavyodhibiti meseji za chuki ambazo tunaziona kila siku katika simu zetu, pia kampuni hizi zimekuwa zikibadili majina kila baada ya muda fulani jambo ambalo pia linakosesha nchi mapato.”
TRA na TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Harry Kitilya alisema kinachowakwamisha ni sheria zilizopo, kwamba wanashindwa kukusanya mapato kwa kuwa kampuni hizo zina misamaha ya kodi.
“Misamaha hii ndiyo inatupa wakati mgumu kukusanya mapato, ila kama sheria hii ya misamaha ya kodi itafanyiwa marekebisho tutaweza kuingia kiasi kikubwa cha kodi,” alisema Kitilya.
Naye Profesa Nkoma alisema ili kuzibana zaidi kampuni za simu kuanzia mwezi Julai mwaka huu utafungwa mtambo maalumu wa kudhibiti mawasiliano (TTMS).