Kampuni kubwa ya teknolojia ya
Apple imesema mauzo ya simu zake zijulikanazo kama iPhone yameanza
kupungua na kwamba mauzo hayo yanatarajiwa kushuka kwa mara ya kwanza
tangu kuzinduliwa kwa simu hizo 2007.
Kampuni hiyo kutoka Marekani
iliuza simu 74.8 milioni robo ya kwanza ya mwaka huu wa kifedha
ikilinganishwa na simu 74.5 milioni robo ya kwanza ya mwaka
uliotangulia. Apple imesema mauzo kutoka kwa robo ijayo yanatarajiwa
kuwa kati ya $50 bilioni na $53 bilioni, kiasi ambacho kitakuwa chini ya
mauzo ya $58 bilioni kipindi sawa mwaka uliotangulia.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mauzo ya iPhone kushuka tangu kuzinduliwa kwa simu hizo za kisasa.
Mauzo ya iPhone yalichangia asilimia 68 ya faina ya kampuni ya Apple mwaka jana.
Kushuka kwa mauzo ya kampuni hiyo kunadaiwa kutokana na kiwango cha uchumi wa China kushuka.
Mauzo
ya Apple nchini China, Hong Kong na Taiwan yaliongezeka 14%, lakini
kiwango hicho cha ukuaji ni cha chini mno kikilinganishwa na ukuaji wa
70% ulioshuhudiwa mwaka mmoja uliopita.
Kampuni ya vifaa vya kielektroniki, Samsung imeathiriwa na kushuka kwa mauzo ya simu zake za aina ya Smartphone.
Mazingira
mabaya ya kibiashara na viwango vya chini vya vifaa vya kiteknolojia
vilisababisha kushuka kwa faida katika robo ya nne ya mwaka jana kwa
asilimia 40 hadi dola bilioni 2.7.
Kampuni hiyo ya Korea Kusini imeonya kwamba itakuwa vigumu kudhibiti faida mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2015.
Mapato ya mwaka 2015 yalishuka hadi dola bilioni 165 ikilinganishwa na miezi 12 iliopita.
Ushindani
mkali kutoka kwa kampuni za Uchina zinazotengeza vifaa rahisi vya
kiteknolojia kama vile Xaiomi na Huwawei katika soko hilo pamoja na
kampuni ya Apple zimeathiri mauzo ya simu za Smartphone.
Simu ya Galaxy S6,ambayo ndio simu ya hadhi ya juu iliozinduliwa
mnamo mwezi Aprili,ilishindwa kuwafurahisha wateja na kampuni hiyo
imeshindwa kudhibiti soko lake.
Jake Saunders,mkurugenzi wa
Asia-Pacific katika kampuni ya utafiti ya ABI Research,ameiambia
BBC:''Inaonyesha kwamba wako chini ya shinikizo kwa sababu nusu ya
mapato yao yanatoka katika simu za rununu''.
Xiaomi inapata wateja
katika soko la India na Indonesia,ambalo ni kubwa kwa simu za
smartphone na ndio eneo ambalo linakuwa kwa haraka.
Kampuni ya usalama mtandaoni ya SplashData imetoa orodha ya nywila au maneno ya siri yaliyotumiwa sana na watu mwaka uliopita.
Orodha hiyo imetayarishwa kwa kutumia maneno ya siri zaidi ya milioni mbili yaliyofichuliwa na wadukuzi mwaka uliopita.
Mwaka
huu, neno ‘Star Wars’, kutoka kwa mwendelezo wa filamu za Star Wars,
lilikuwa miongoni mwa maneno 25 yaliyotumiwa zaidi. Filamu ya Star Wars:
The Force Awakens ilizinduliwa mwezi Desemba.
Wengi bado wanatumia ‘123456’ kama nywila na wengine ‘password’. Ili kuwa salama mtandaoni, huwa ni vyema kutumia nyila ambayo watu wengine hawawezi wakaifikiria au kugundua kwa urahisi.
Moja ya njia za kuimarisha neno la siri ni kuchanganya tarakimu, herufi na alama pamoja na kuchanganya herufi kubwa na ndogo.
Lakini wengi hutatizika katika kukumbuka nywila.
Moja ya njia unazoweza kutumia ni kuangalia maneno ya wimbo uupendao na kuyafupisha.
Hapa kuna mfano wa jinsi unaweza kupata nyila kutoka kwa wimbo.
Chagua mwanamuziki umpendaye, tuseme
Chagua wimbo wake
Tafuta mstari mmoja, sana ukupendezao zaidi,
Fupisha kwa kuchukua herufi ya kwanza
ya kila neno, au herufi mbili za kwanza. Tukichukua herufi mbili za
kwanza.
Changanya herufi kubwa na ndogo
Kisha, badilisha herufi zinazokaribiana na tarakimu kuwa tarakimu, mfano badala ya ‘a’ tumia ‘@’ na badala ya ‘i’ tumia ‘1’.
Ni vigumu mtu
kuigundua kwa urahisi lakini kila ukikumbuka wimbo wako unaweza
ukaikumbuka kwa urahisi.
Vifaa vya mawasiliano vya mkononi –
hususan simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) –
vina namba maalum inayovitambulisha. Namba hiyo inajulikana kama IMEI ambacho
ni kifupi cha International Mobile Equipment Identity.
Kifungu cha 84 cha Sheria ya
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka kuwepo kwa mfumo
wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Rajisi
hii inajulikana kwa kiingereza kama Central Equipment Identification Register,
kwa kifupi CEIR. Sheria inataka rajisi hiyo ihifadhiwe na kuendeshwa na Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania.
Aidha Kanuni za mwaka 2011 za EPOCA
kuhusu mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya
mkononi inawataka watoa huduma wa mawasiliano yanayotumia vifaa vya mkononi
kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi (Equipment Identity
Register – EIR) za vifaa vya mkononi vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Mfumo huu wa kielektroniki ambao
utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi
una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika,
kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Vifaa vyote vya mawasiliano vya
mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya
matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza kufanya kazi kwenye mitandao ya
mawasiliano kutumia vifaa vya mkononi.
UFAFANUZI
Taarifa kwenye mfumo huu wa rajisi zitakuwa na aina tatu za kumbukumbu; ambazo
ni orodha ya namba tambulishi ambazo vifaa vyake vinaruhusiwa, orodha ya namba
tambulishi ambazo zimetolewa taarifa kuwa zimefungiwa na namba tambulishi
ambazo zimefungiwa kwa muda au kuruhusiwa kwa muda.
Orodha Nyeupe:
Orodha ya vifaa vya mkononi vya mawasiliano vinavyoruhusiwa kutumika katika
mitandao ya huduma za simu za kiganjani
Orodha Nyeusi:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa na mtoa huduma kwenye
mfumo wao wa EIR na kutumwa kwenye mfumo wa CEIR kwa ajili ya kufungiwa ili
zisitumike kwenye mitandao mingine ya simu za kiganjani kwa mujibu wa utaratibu
uliowekwa na kukubaliwa miongoni mwa watoa huduma. Simu zote za mkononi
zilizoibiwa au kupotea zitafungiwa ndani ya saa 24 ili zisitumike kwenye
mtandao wowote wa simu za mkononi Tanzania.
Ikitokea simu ya mtumiaji ikafungiwa
kinamosa, anatakiwa kutoa taarifa mara moja kwa mtoa huduma wako kwa ajili ya
kuifungua. Watoa huduma wanatakiwa wafungulie, ndani ya saa 24, simu zote
zilizofungwa kimakosa.
Orodha ya kijivu:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa au kufunguliwa kwa muda
kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuzifuatilia.
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na
akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye
mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima
adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya angalau miezi 12. Mteja
anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo
simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho
mbadala wa milki ya simu husika.
2. Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu
cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au
kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu
kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu
mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha
Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio,
maarufu kama RB.
Anatakiwa aende kwa mtoa huduma
kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu
iliyopotea ( risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo). Mtoa huduma
kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na atampatia mteja namba
ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa isutumike kwenye mitandao ya simu na
hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa 24.
3. Kujenga misingi ya matumizi ya
simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo
inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.
KUTAMBUA NAMBA TAMBULISHI
Ili kutambua namba tambulishi ya simu ya kiganjani au vifaa vya mawasiliano ya
kiganjani, mtumiaji anatakiwa aandike tarakimu *#06# kwa kutumia kifaa chake.
Baada ya kufanya hivyo, kutaonekana namba ndefu. Mtumiaji anatakiwa kuandika
namba hiyo kama ilivyoonekana kwenye kifaa chakena kuihifadhi katika hali ya
usalama kwa ajili ya rejea ya baadae.
Baada ya hapo mtumiaji atume ujumbe
mfupi wenye hiyo namba tambulishi kwenda namba 15090. Atapokea meseji
itakayomjulisha kuhusu hali halisi ya simu yake ya kiganjani. Mtumiaji atapokea
ujumbe kuhusu uhalisia wa simu yake. Majibu yatakayokuja yatasomeka: Kama IMEI
haioani na aina ya simu yako, wasiliana na aliyekuuzia. Usipoweza,ibadilishe
kabla ya Juni 2016 kwani simu hiyo inaweza kuwa BANDIA.
HATUA ZA KUCHUKUA IWAPO SIMU
ITAONEKANA HAIKIDHI VIWANGO, SI HALISI NA NI BANDIA
Mtu yeyote ambaye atatambua kwamba
simu yake ya kiganjani si halisi,ni bandia na haikidhi viwango atapewa muda wa
kuendelea kutumia simu hiyo. Baada ya muda huo kumalizika, simu hiyo itaingizwa
katika orodha nyeusi na kufungiwa isitumike kwenye mitandao mingine yoyoye ya
simu za kiganjani.
Watumiaji wote wenye simu za
kiganjani ambazo namba tambulishi zao zinaonyesha kwamba simu hizo si halisi,
ni feki na hazikidhi viwango watagharamia ununuzi wa simu nyingine.
Watumiaji wote ambao namba
tambulishi za simu zao zinaonyesha kwamba vifaa hivyo si halisi, ni feki na
havikidhi viwango watatakiwa kubadilisha simu hizo na kupata zinazokidhi
viwango na halisi katika muda wa miezi sita kuanzia siku ya uzinduzi wa mfumo
wa rajisi ya namba za utambulisho wa simu za kiganjani.
Ni vyema ifahamike kwamba simu zote
za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) ambazo zitakuwa
na namba tambulishi bandia zitafungiwa kuanzia 16 Juni 2016.
HITIMISHO
Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi
una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo
vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya
kiganjani (tablets). Uanzishwaji wake ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya Sheria
ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010. Ni vyema watumiaji
wakazingatia maelekezo kuhusu utaratibu wa kuhakiki namba tambulishi, kutoa
taarifa wanapopoteza au kuibiwa simu.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
18 December 2015
Wakaazi bilioni 4.2 wa dunia hawana njia ya kutumia mtandao wa Intaneti. Idadi hiyo ni sawa na asili mia 60 ya wakaazi wa dunia-benki kuu ya
dunia imesema hayo mjini Washington.
Kumeibuka "pengo la digitali"
kutokana na ule ukweli kwamba intanet inakutikana zaidi katika nchi
tajiri.
Nchini India watu bilioni moja nukta moja hawana mtandao wa
intaneti,nchini China wanafikia watu milioni 755 na Indonesia watu
milioni 213.
Pengo hilo linazidi kuwa pana linapohusika suala la
intaneti ya haraka-inasema benki kuu ya dunia.
Wanaofaidika na
intaneti kama hiyo ni watu bilioni moja nukta moja tu-ikimaanisha chini
ya asilimia 15 ya wakaazi jumla wa dunia.
"Watu wanabidi wajiepushe
isiibuke "tabaka mpya ya wanaobaguliwa kijamii" anaonya mwanauchumi mkuu
wa benki kuu ya dunia Kaushik Basu katika ripoti yake iliyopewa jina
"Faida ya teknolojia ya habari."
Mitandao ya whatsapp na viber huenda
ikadhibitiwa Afrika Kusini ikitegemea matokeo ya vikao vya bunge
baadaye mwezi huu, umeripoti mtandao unaoheshimika wa Fin24.
Umaarufu
wa Whatasap inayomilikiwa na facebook umeongezeka nchini Afrika Kusini
ukiwa na watumiaji Zaidi ya milioni kumi kwa mujibu wa ripoti ya World
Wide Worx na Fuseware.
Kampuni mbili kubwa za simu Afrika kusini Vodacom na MTN mwaka uliopita zilitoa wito wa kudhibitiwa kwa huduma hizo.
Kuna hawa washiriki wanaopata manufaa makubwa katika sekta hii bila
kutumia pesa. Tutapataje usawa?" afisa mmoja wa MTN alinukuliwa akisema.Kamati
ya bunge kuhusu mawasiliano ya posta ilipanga kufanya kikao hicho
tarehe 26 mwezi January kujadili sera za kuingilia kati swala hilo. Chanzo:BBC
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura
(kushoto) akibadilishana hati ya makubaliano ya mkopo na Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Uwekezaji (TIB), Jaffer Machano mara
baada ya kutiliana saini.
Kampuni
ya Simu Tanzania TTCL na Benki ya TIB zimetiliana saini Mkataba wa
makubaliano ya dhamana ya Benki na Mkopo wa Dola za Marekani Milioni 22 ikiwa ni
awamu ya kwanza ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 329 itakazopewa TTCL.
Akizungumza
katika hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya mkopo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu
wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema mkopo huo ni mahususi kwa ajili ya
kuiwezesha TTCL kusimika mitambo mipya na ya kisasa kuboresha huduma zake kwa
kujenga na kusambaza huduma za Mitandao
ya 3G na 4G LTE nchini kote.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Jaffer Machano
amesema katika kutimiza wajibu wa TIB kama benki ya maendeleo, ujenzi wa
miundombinu umepewa kipaumbele na hii ni pamoja na miundombinu ya sekta ya Mawasiliano.
Baadhi ya huduma za TTCL zitakazoimarika
baada ya uwezeshaji huu ni pamoja huduma za simu na intaneti yenye kasi kubwa
inayowezesha huduma za kijamii kufanyika kwa urahisi kwa njia ya mtandao.
Huduma kama vile za Elimu kwa njia ya mtandao (E education), Afya kwa njia ya
mtandao (E health) na huduma katika Sekta nyingine za kiuchumi kama vile Biashara,
Viwanda na Kilimo nazo zitanufaika sana ambapo wafanyabiashara na wazalishaji
wa bidhaa mbalimbali watapata Mawasiliano ya uhakika katika kufanikisha
shughuli zao.
Kampuni ya Simu Tanzania TTCL ipo
mbioni kuanzisha huduma ya kusafirisha fedha kwa njia ya Mtandao ifikapo robo
ya pili ya mwaka huu ili kutekeleza ombi la muda mrefu la Wateja wake
wanaohitaji sana kuanzishwa kwa huduma hii kutokana na Mtandao mpana wa Kampuni
uliosambaa ndani na nje ya nchi na unafuu wa gharama.
Twitter ina mpango wa kuongeza
kiwango cha idadi ya herufi zinazoandikwa katika nafasi ya ujumbe kutoka
140 hadi 10,000 sawa na ujumbe wa kawaida.
Baada ya uvumi mtandao huo sasa umeamua kuongeza idadi hiyo.
Ni hatua ya hivi karibuni ya Twitter kuweza kuwavutia wateja zaidi.
Mkuu wa Twitter na mwanzilishi Jack Dorsey amesema kuwa ataongeza idadi ya kiwango cha herufi zitakazotumika.
Iwapo Twitter itakubali kiwango cha ujumbe wenye herufi 10,000 huenda ikazalisha ujumbe wa maneno 1,700.
Katika
ujumbe wake ,Jack Dorsey ameandika kwamba Twitter tayari imebaini
kwamba wengi wa wateja wake milioni 300 tayari wamekuwa wakipiga picha
kubwa za ujumbe mrefu katika ujumbe wao.
Amesema kuwa Twitter inajaribu kutafuta mbinu za kuwapa watu zaidi uwezo wa kujielezea bila kuchafua huduma hiyo. Chanzo:BBC
Wadau mbalimbali wa mitandao ya kijamii
jijini Arusha wameeleza kuwa, Elimu duni kuhusu matumizi ya mtandao ndio chanzo
cha matumizi mabaya ya mitandao hiyo hali inayosababisha migogoro katika jamii.
Akizungumzia suala hilo Bwana Fransis
Kimati ameeleza kuwa elimu duni kuhusu mitandao ikiwemo ukuaji wa sayansi na
Teknolojia ndio chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili hususani kwa vijana.
Kwa upande wake Bw. Joshua Jacob
ambaye ni mwandishi wa vitabu amesema, hatua zinataikiwa kuchukuliwa ikiwemo
utolewaji elimu kwa rika la vijana ambao ndio kundi kubwa la watumiji wa
mitandao, kupitia vitabu, majarida warsha na matamasha mbalimbali, ili
kubadilisha mitazamo mibaya kwa vijana.
Aidha wamesema kuwa dhamira ya kuwepo
mitandao ya kijamii mbalimbali ikiwemo Facebook,Twiter ni nzuri lakini bado
jamii haijawa na ufahamu wa kutumia mitandao hiyo kwa kujiendeleza katika
njanja mbalimbali.