Thursday, April 7, 2016

WHATSAPP YALINDA UJUMBE WA WATUMIAJI WAKE

 

Huduma ya ujumbe Whatsapp imetangaza kuwa itayalinda mawasiliano ya wateja wake kuanzia hapo siku ya Jumanne April 5,mwaka huu

Huku ulinzi ukiwekwa mwanzo na mwisho wa ujumbe ,ujumbe hautaharibiwa wakati unapotoka katika simu ya anayeutuma na unaweza kusomwa pekee na anayeupokea.

Hatua hiyo itaufanya ujumbe huo kutosomeka iwapo mhalifu ama hata maafisa wa polisi wanajaribu kuingilia simu bila idhini.

WhatsApp ambayo ina wateja zaidi ya bilioni moja duniani imesema kuwa uhamisho wa faili pamoja na sauti pia zitalindwa.

Huduma hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Facebook imesema kuwa ulinzi wa mawasiliano ya faragha ni miongoni mwa malengo yake.

Ulinzi huo uliathiriwa wakati shirika la Marekani la FBI lilipotaka kampuni ya Apple kuisadia kuchukua data katika simu moja ya iphone iliotumiwa na muuaji Syed Farook.

Whatsapp ilisema:Wazo hilo ni rahisi, unapotuma ujumbe mtu pekee anayeweza kuusoma ni mtu ama kundi la mawasiliano ambalo umelitumia ujumbe huo.

Hakuna mtu anayeweza kuusoma ujumbe huo hata kama ni wahalifu wa mitandaoni ama hata serikali.hata sisi hatuwezi kuusoma.

Watumiaji wapya wa huduma hiyo waliarifiwa kuhusu mabadiliko hayo wakati wanapotuma ujumbe siku ya Jumanne ya April 5,mwaka huu

Wednesday, April 6, 2016

NJIA ZINAZOTUMIWA NA WAFANYABIASHARA WA SIMU KUKWEPA USHURU NCHINI TANZANIA


 

Utafiti uliofanywa mwaka jana na Kampuni ya Utengenezaji wa simu ya Nokia kabla haijabadilishwa na kuwa Microsoft kuhusu biashara ya mauzo ya simu katika nchi mbalimbali barani Afrika,Tanzania ikiwa ni miongoni mwao,umebaini kuwa kuna mianya ambayo imekuwa ikitumika kuingiza simu hizo kwa njia za magendo bila kulipia ushuru huku ukiikosesha Serikali ya Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 91.23.

Utafiti huo unaeleza kuwa njia ambazo zimekuwa zikitumika ni upitishaji wa simu katika maeneo ya pembezoni mwa nchi hususani mikoa iliyoko mipakani mwa Tanzania na nchi jirani na kuingiza simu za magendo kupitia katika viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam na ule wa Kilimanjaro ambapo wafanyabiashara hulipia kiasi kidogo cha fedha ambazo hukadiliwa bila kuangalia uzito na thamani ya mzigo alionao.

Takwimu za utafiti huo zinaonesha kuwa kwa wastani,simu za kawaida takribani 750,000 huuzwa kwa mwezi nchini Tanzania ambapo wastani wa bei kwa simu moja ni Sh 35,000 ambapo jumla ya mauzo ni Sh bilioni 26.2,huku kwa upande wa simu za kisasa kwa mwezi zikiuzwa simu 87,000 na wastani wa bei ikiwa ni Sh 250,000 ambapo mauzo yake kwa mwezi ni sawa na Sh bilioni 21.75.

Jumla ya simu zinazouzwa kwa mwezi ni 837,000 ambapo thamani yake ni Sh Bilioni 48,kama zimu zote zitalipiwa ushuru wa asilimia 18 na mianya yote kufungwa basi serikali inastahili kukusanya Sh.Bilioni 8.64 kwa mwezi.

Thursday, March 31, 2016

WAHALIFU MTANDAO WADUKUA TOVUTI 20 ZA SERIKALI NCHINI ANGOLA

 

Kikundi cha kihalifu mtandao cha ‪#‎Anonymous‬ kimetekeleza mashambulizi mtandao dhidi ya Nchi ya Angola na kufanikiwa kudukua na kuangusha Tovuti 20 za serikali ya Nchi Hiyo.

Hatua hiyo ya kikundi hicho imefuatia baada ya kushinikiza serikali ya Nchi hiyo kuwaachia watu 17 waliokamatwa kutokana na uasi dhidi ya Serikali ya Rais Jose Eduardo dos Santo.


Tukio hilo la Mashambulizi limepokelewa kwa masikitikomakubwa na jumuia ya wana usalama mitandao huku usaidizi wa dhati kuimarisha usalama kwa tovuti za Nchi hiyo zikichukuliwa.


Matukio ya kushambulia Serikali za Nchi za Afrika kimtandao yamepata kuonekana mara kadhaa ambapo Ghana pia ilipata kua muathirika.

Thursday, March 3, 2016

WHATSAPP NAYO YATANGAZA KUTOTUMIKA KATIKA BAADHI YA MATOLEO YA SIMU DUNIANI IFIKAPO DISEMBA 2016

 WhatsApp

Baada ya Serikali ya Tanzania kuanzisha kampeni ya kuondosha matumizi ya simu zisizohalisi toka Disemba mwaka jana,ambapo simu hizo hazitaendelea kutumika ifikapo Juni mwaka 2016 huku ikielezwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuwa kuna asimilia 40 ya simu zinazotumika nchini humo ambazo ni halisi. TCRA na Makampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Simu za Mkononi Tanzania kwa sasa wanaendesha kampeni ya kuhakiki simu ya mtumiaji kama ni halisi ama si halisi kwa kutumia IMEI ya simu kuituma kwenda namba 15090.

Mtandao wa kijamii wa WhatsApp ulio na watumiaji bilioni moja duniani katika mawasilino miongoni mwao wakiwemo watanzania,nao hauko nyuma katika kutafuta kilichobora kwai umetangaza kuwa ifikapo Disemba 2016 hatutatumika katika baadhi ya simu zilizopo duniani.

Huduma ya WhatsApp haitatumika tena katika simu zinazotumia mifumo kadha ya programu endeshi ikiwemo Blackberry 10, Nokia Symbian S60 na Windows Phone 7.1.
Kampuni ya Facebook inayomiliki huduma hiyo imesema inataka kuangazia kustawisha “huduma katika mifumo inayotumiwa na watu wengi.

Kampuni hiyo imejitetea na kusema kwamba haijawatupa wateja wake ambao wamechangia sana katika ufanisi wake lakini ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Orodha kamili ya mifumo ya simu ambayo wateja hawataweza tena kutumia WhatsApp ni hii hapa:
  • Android 2.1 and Android 2.2
  • Blackberry OS 7 and earlier
  • Blackberry 10
  • Nokia S40
  • Nokia Symbian S60
  • Windows Phone 7.1
Kampuni hiyo imesema wakati wa kuanzishwa kwa WhatsApp mwaka 2009, asilimia 70 ya simu wakati huo zilikuwa za BlackBerry na Nokia."

Lakini sasa asilimia 99.5 ya simu zinatumia mifumo ya Google, Apple na Microsoft.
Chanzo:BBC

Thursday, February 18, 2016

TTCL YAKANUSHA MFUMO WAKE WA MAWASILIANO KUDUKULIWA

 http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2016/02/IMG_0142.jpg
 Meneja Uhusiano wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Thomas Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam kukanusha taarifa za kampuni hiyo kudukuliwa.

 http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2016/02/IMG_0182.jpg
Meneja wa Kitengo cha Usalama Mifumo ya Mawasiliano ya TTCL, Lina Rujweka akifafanua jambo kwenye mkutano na vyombo vya habari.

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa mfumo wa mawasiliano wa kampuni hiyo umeingiliwa na wadukuzi. Taarifa iliyotolewa juma hili kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Nicodemus Thomas Mushi alisema taarifa zinazotolewa si za kweli hivyo kuwataka wateja wao wazipuuze.



 “Tunapenda kuwathibithia Wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi, wadau wetu na Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si sahihi, na kwamba mifumo yetu ya Mawasiliano ya TTCL ipo salama, huduma zetu zote zipo thabiti na mpaka sasa tunapotoa taarifa hii, hakuna uhalifu wowote uliofanyika kwa sisi wenyewe kama Kampuni wala kwa mteja wetu yeyote,” alisema Thomas Mushi.



Aidha, tunapenda kuwathibitishia kuwa, taarifa za Wateja wetu wote ikiwemo Serikali , Idara, Wakala na Taasisi za Umma, Taasisi za fedha, Mashirika, Makampuni na Watu binafsi zipo salama kabisa. Ukweli huu unathibitishwa na Wateja wao pia kwani hadi sasa, hakuna hata mmoja aliyeleta taarifa za kukosa huduma ama kupata athari zozote kutokana na tetesi hizo.



Hata hivyo, alisema pamoja na taarifa hizo, Wataalamu wa kampuni hiyo wanaendelea kuwa macho kwa muda wote, ili kuhakikisha kuwa, wanafanyia kazi kila taarifa ama tishio la kiusalama linaloweza kujitokeza katika mfumo wao.



“TTCL inaendelea kuwaomba Umma na Wateja wetu wote kuendelea na majukumu yao kama kawaida bila wasiwasi wowote. TCCL inawaleta Karibu.” Alisema Thomas Mushi.



Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha Usalama Mifumo ya Mawasiliano ya TTCL, Lina Rujweka alisema kitengo chao baada ya tetesi hizo kimefanya uchunguzi wa kina na hakuna ashirio lolote la mifumo yao kuingiliwa (kudukuliwa) kama ilivyoelezwa.



Alisema kitengo hicho kina wataalam ambao muda wote wapo kazini kufuatilia ufanisi wa mfumo wa mawasiliano wa kampuni yao hivyo kuwaondoa hofu wateja wao.



“Baada ya taarifa hizo Kitengo cha Usalama wa Mifumo ya Mawasiliano ya Kampuni ya TTCL kiliingia kazini ili kubaini ukweli wa taarifa hizo na kufanya majaribio ya kitaalamu ili kuthibitisha usalama wa mifumo yetu. Baada ya utafiti wa kina na majaribio ya kitaalamu, tunapenda kuwathibithia Wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi, wadau wetu na Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizi si sahihi...” alisema.

Tuesday, February 16, 2016

TIGO YATAHADHARISHA WATEJA DHIDI YA MATUMIZI YA SIMU BANDIA

Mkuu wa  Kitengo cha Vifaa vya Mawasiliano wa TigoDavid Zakaria akielezea athari  za matumizi ya  simu bandia kwa waandishi wa habari  (Hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika mapema leo katika makao makuu ya Tigo Kijitonyama Dar es salaam., kushoto kwake ni Meneja wa Mawasiliano, John Wanyancha
 Watumiaji wa simu za mkononi wameonywa dhidi ya matumizi ya simu bandia na zisisokidhi viwango vya ubora ambazo tayari zimetangwa kupigwa marufuku na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

Kutokana na sababu hiyo, Tigo, ambayo ni kampuni ya kidijitali, imeanza kuendesha kampeni ya kuhamasisisha wateja wake na umma kwa jumla kupitia vyombo vya Habari inayolenga kuwaepusha na athari za matumizi ya simu bandia.

Kwa mujibu wa maelekezo ya TCRA matumizi ya simu za mkononi ambazo namba zake za utambulisho wa kimataifa (IMEI) ni bandia yatapigwa marufuku kutumika kwa mitandao yote ya simu nchini Tanzania kuanzia Juni 16 mwaka huu. Ili kujiepusha na usumbufu wowote utakaotokana na hatua hii tunawashauri wateja wetu kujipatia simu halisi na bora kutoka maduka ya Tigo yaliyo karibu nao,`` alisema Mkuu wa  Kitengo cha Vifaa vya Mawasiliano wa Tigo, David Zakaria.
Ripoti ya utafiti ulichapishwa katika tovuti ya GSMA ("http://www.gsma.com" www.gsma.com ) inasema kwamba tofauti na ilivyo kwa simu halali ambazo hupitia mamia ya hatua mbalimbali za kuhakiki ubora wake kabla ya kupelekwa sokoni, simu bandia hazifanyiwi majaribio ya ubora na kuna taarifa za kitafiti zinazoonyesha kuwa baadhi ya simu bandia zina kiwango kikubwa cha madini ya risasi na vitu vingine ambavyo ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa simu feki zinatengenezwa na malighafi dhaifu zisizokidhi viwango na zimeshaonesha kuwa kiwango cha hatari cha vyuma na kemikali kama risasi hadi kufikia kiwango cha mara 40 zaidi kuliko kiwango kilichoidhinishwa na sekta ya mawasiliano duniani kwa mujibu wa na Jukwaa la Watengenezaji wa Simu za Mkononi (MMF).

Akizungumza kuhusu hatua ya Tigo kutoa tahadhari kwa wateja wake Zakaria alisema, ``Wanunuzi wanatakiwa kuwa waangalifu wakati wanaponunua simu mpya au vifaa vya mawasiliano madukani au katika intaneti kwa sababu bidhaa nyingi feki zinatengenezwa kwa kuigaa muundo na nembo za kibiashara za bidhaa halisi kwa makusudi ili kuwalaghai wateja. 

``Ili kuweza kuelewa iwapo simu yako ni feki au ni halisi unatakiwa kupiga namba namba *#06# ambapo atapokea  namba ya IMEI ya simu hiyo na kisha kutima kwa njia ya jumbe mfupi kwenda namba 15090 ambapo utapata jibu iwapo simu hiyo ya mkononi ni halisi au ni bandia,” alisema Zacharia.

Wednesday, February 3, 2016

TCRA YATOA SEMINA KWA WAANDISHI WA HABARI KUGUNDUA SIMU FEKI

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Innocent Mungy, akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar kuhusiana na kutambua Simu Feki na kudhibiti uingiaji wa Simu hizo Tanzania na kueleza mwisho wa matumizi wa simu hizo Nchini Tanzania ni Juni 2016. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilima Zanzibar na kuwashirikisha waandishi wa Vyombo mbali mbali vilioko Zanzibar. 
Naibu Mkurugenzi Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano  TCRA Thadayo Ringo, akizungumza na waandishi wa habari jinsi ya kutambua Simu feki wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari Zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar, Amesema utambuzi wa kujua simu yako kama ni orijinali  unaweza kupiga namba kuaza na Nyota Reli 06 Reli . *# 06#  na utapata ujumbe wa Simu yako kwa Mfano zitakuja tarakimu 15  mfano   IMEI 12456789067654  Na Kupiga 15090 Ujumbe wa kukuelewesha kama ni simu yako orijino. kwa mfano kama huu Sony Mobile Communications AB -SONY  C5555 - Xperia. huu ni mfano wa kujua simu orijino.
Naibu Mkurugenzi Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Thadayo Ringo akionesha mfano wa simu orijino kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo wa TCRA uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar.
Imetayarishwa na Othman Mapara.Blogspot

Thursday, January 28, 2016

IPHONE YAPOROMOKA SOKONI

 

Kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple imesema mauzo ya simu zake zijulikanazo kama iPhone yameanza kupungua na kwamba mauzo hayo yanatarajiwa kushuka kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa simu hizo 2007.

Kampuni hiyo kutoka Marekani iliuza simu 74.8 milioni robo ya kwanza ya mwaka huu wa kifedha ikilinganishwa na simu 74.5 milioni robo ya kwanza ya mwaka uliotangulia. Apple imesema mauzo kutoka kwa robo ijayo yanatarajiwa kuwa kati ya $50 bilioni na $53 bilioni, kiasi ambacho kitakuwa chini ya mauzo ya $58 bilioni kipindi sawa mwaka uliotangulia.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mauzo ya iPhone kushuka tangu kuzinduliwa kwa simu hizo za kisasa.

Mauzo ya iPhone yalichangia asilimia 68 ya faina ya kampuni ya Apple mwaka jana.

Kushuka kwa mauzo ya kampuni hiyo kunadaiwa kutokana na kiwango cha uchumi wa China kushuka.

Mauzo ya Apple nchini China, Hong Kong na Taiwan yaliongezeka 14%, lakini kiwango hicho cha ukuaji ni cha chini mno kikilinganishwa na ukuaji wa 70% ulioshuhudiwa mwaka mmoja uliopita.

MAUZO YA SIMU ZA KISASA (SMARTPHONE) ZA SAMSUNG YASHUKA


 
Kampuni ya vifaa vya kielektroniki, Samsung imeathiriwa na kushuka kwa mauzo ya simu zake za aina ya Smartphone.

Mazingira mabaya ya kibiashara na viwango vya chini vya vifaa vya kiteknolojia vilisababisha kushuka kwa faida katika robo ya nne ya mwaka jana kwa asilimia 40 hadi dola bilioni 2.7.

Kampuni hiyo ya Korea Kusini imeonya kwamba itakuwa vigumu kudhibiti faida mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2015.

Mapato ya mwaka 2015 yalishuka hadi dola bilioni 165 ikilinganishwa na miezi 12 iliopita.

Ushindani mkali kutoka kwa kampuni za Uchina zinazotengeza vifaa rahisi vya kiteknolojia kama vile Xaiomi na Huwawei katika soko hilo pamoja na kampuni ya Apple zimeathiri mauzo ya simu za Smartphone.

Simu ya Galaxy S6,ambayo ndio simu ya hadhi ya juu iliozinduliwa mnamo mwezi Aprili,ilishindwa kuwafurahisha wateja na kampuni hiyo imeshindwa kudhibiti soko lake.

Jake Saunders,mkurugenzi wa Asia-Pacific katika kampuni ya utafiti ya ABI Research,ameiambia BBC:''Inaonyesha kwamba wako chini ya shinikizo kwa sababu nusu ya mapato yao yanatoka katika simu za rununu''.

Xiaomi inapata wateja katika soko la India na Indonesia,ambalo ni kubwa kwa simu za smartphone na ndio eneo ambalo linakuwa kwa haraka.

Wednesday, January 20, 2016

NYWILA ZILIZOTUMIWA SANA NA WATU MWAKA 2015

Kampuni ya usalama mtandaoni ya SplashData imetoa orodha ya nywila au maneno ya siri yaliyotumiwa sana na watu mwaka uliopita.

Orodha hiyo imetayarishwa kwa kutumia maneno ya siri zaidi ya milioni mbili yaliyofichuliwa na wadukuzi mwaka uliopita.

Mwaka huu, neno ‘Star Wars’, kutoka kwa mwendelezo wa filamu za Star Wars, lilikuwa miongoni mwa maneno 25 yaliyotumiwa zaidi. Filamu ya Star Wars: The Force Awakens ilizinduliwa mwezi Desemba.

Wengi bado wanatumia ‘123456’ kama nywila na wengine ‘password’.
Ili kuwa salama mtandaoni, huwa ni vyema kutumia nyila ambayo watu wengine hawawezi wakaifikiria au kugundua kwa urahisi.

Moja ya njia za kuimarisha neno la siri ni kuchanganya tarakimu, herufi na alama pamoja na kuchanganya herufi kubwa na ndogo.

Lakini wengi hutatizika katika kukumbuka nywila.

Moja ya njia unazoweza kutumia ni kuangalia maneno ya wimbo uupendao na kuyafupisha.

Hapa kuna mfano wa jinsi unaweza kupata nyila kutoka kwa wimbo.
  1. Chagua mwanamuziki umpendaye, tuseme
  2. Chagua wimbo wake
  3. Tafuta mstari mmoja, sana ukupendezao zaidi,
  4. Fupisha kwa kuchukua herufi ya kwanza ya kila neno, au herufi mbili za kwanza. Tukichukua herufi mbili za kwanza.
  5. Changanya herufi kubwa na ndogo
  6. Kisha, badilisha herufi zinazokaribiana na tarakimu kuwa tarakimu, mfano badala ya ‘a’ tumia ‘@’ na badala ya ‘i’ tumia ‘1’.
 Ni vigumu mtu kuigundua kwa urahisi lakini kila ukikumbuka wimbo wako unaweza ukaikumbuka kwa urahisi.

 Nywila zilizotumiwa sana 2015
1. 123456
2. password
3. 12345678
4. qwerty
5. 12345
6. 123456789
7. football
8. 1234
9. 1234567
10. baseball
11. welcome
12. 1234567890
13. abc123
14. 111111
15. 1qaz2wsx
16. dragon
17. master
18. monkey
19. letmein
20. login
21. princess
22. qwertyuiop
23. solo
24. passw0rd
25. starwars
Chanzo:BBC

Saturday, January 16, 2016

KUMBUKA TCRA ILISHATOA MUDA WA MIEZI SITA KUZIFUNGA SIMU FEKI NCHINI TANZANIA ANGALIA VIDEO NA MAELEZO



UTANGULIZI:

Vifaa vya mawasiliano vya mkononi – hususan simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) – vina namba maalum inayovitambulisha. Namba hiyo inajulikana kama IMEI ambacho ni kifupi cha International Mobile Equipment Identity.


Kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka kuwepo kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Rajisi hii inajulikana kwa kiingereza kama Central Equipment Identification Register, kwa kifupi CEIR. Sheria inataka rajisi hiyo ihifadhiwe na kuendeshwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.


Aidha Kanuni za mwaka 2011 za EPOCA kuhusu mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi inawataka watoa huduma wa mawasiliano yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi (Equipment Identity Register – EIR) za vifaa vya mkononi vinavyotumika kwenye mitandao yao.


Mfumo huu wa kielektroniki ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.


Vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza kufanya kazi kwenye mitandao ya mawasiliano kutumia vifaa vya mkononi.


UFAFANUZI
Taarifa kwenye mfumo huu wa rajisi zitakuwa na aina tatu za kumbukumbu; ambazo ni orodha ya namba tambulishi ambazo vifaa vyake vinaruhusiwa, orodha ya namba tambulishi ambazo zimetolewa taarifa kuwa zimefungiwa na namba tambulishi ambazo zimefungiwa kwa muda au kuruhusiwa kwa muda.


Orodha Nyeupe:
Orodha ya vifaa vya mkononi vya mawasiliano vinavyoruhusiwa kutumika katika mitandao ya huduma za simu za kiganjani


Orodha Nyeusi:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa na mtoa huduma kwenye mfumo wao wa EIR na kutumwa kwenye mfumo wa CEIR kwa ajili ya kufungiwa ili zisitumike kwenye mitandao mingine ya simu za kiganjani kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na kukubaliwa miongoni mwa watoa huduma. Simu zote za mkononi zilizoibiwa au kupotea zitafungiwa ndani ya saa 24 ili zisitumike kwenye mtandao wowote wa simu za mkononi Tanzania.


Ikitokea simu ya mtumiaji ikafungiwa kinamosa, anatakiwa kutoa taarifa mara moja kwa mtoa huduma wako kwa ajili ya kuifungua. Watoa huduma wanatakiwa wafungulie, ndani ya saa 24, simu zote zilizofungwa kimakosa.

Orodha ya kijivu:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa au kufunguliwa kwa muda kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuzifuatilia.

FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya angalau miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.


2. Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB.

Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea ( risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo). Mtoa huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa 24.


3. Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.


KUTAMBUA NAMBA TAMBULISHI
Ili kutambua namba tambulishi ya simu ya kiganjani au vifaa vya mawasiliano ya kiganjani, mtumiaji anatakiwa aandike tarakimu *#06# kwa kutumia kifaa chake. Baada ya kufanya hivyo, kutaonekana namba ndefu. Mtumiaji anatakiwa kuandika namba hiyo kama ilivyoonekana kwenye kifaa chakena kuihifadhi katika hali ya usalama kwa ajili ya rejea ya baadae.


Baada ya hapo mtumiaji atume ujumbe mfupi wenye hiyo namba tambulishi kwenda namba 15090. Atapokea meseji itakayomjulisha kuhusu hali halisi ya simu yake ya kiganjani. Mtumiaji atapokea ujumbe kuhusu uhalisia wa simu yake. Majibu yatakayokuja yatasomeka: Kama IMEI haioani na aina ya simu yako, wasiliana na aliyekuuzia. Usipoweza,ibadilishe kabla ya Juni 2016 kwani simu hiyo inaweza kuwa BANDIA.


HATUA ZA KUCHUKUA IWAPO SIMU ITAONEKANA HAIKIDHI VIWANGO, SI HALISI NA NI BANDIA

Mtu yeyote ambaye atatambua kwamba simu yake ya kiganjani si halisi,ni bandia na haikidhi viwango atapewa muda wa kuendelea kutumia simu hiyo. Baada ya muda huo kumalizika, simu hiyo itaingizwa katika orodha nyeusi na kufungiwa isitumike kwenye mitandao mingine yoyoye ya simu za kiganjani.


Watumiaji wote wenye simu za kiganjani ambazo namba tambulishi zao zinaonyesha kwamba simu hizo si halisi, ni feki na hazikidhi viwango watagharamia ununuzi wa simu nyingine.


Watumiaji wote ambao namba tambulishi za simu zao zinaonyesha kwamba vifaa hivyo si halisi, ni feki na havikidhi viwango watatakiwa kubadilisha simu hizo na kupata zinazokidhi viwango na halisi katika muda wa miezi sita kuanzia siku ya uzinduzi wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa simu za kiganjani.


Ni vyema ifahamike kwamba simu zote za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) ambazo zitakuwa na namba tambulishi bandia zitafungiwa kuanzia 16 Juni 2016.

HITIMISHO
Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets). Uanzishwaji wake ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010. Ni vyema watumiaji wakazingatia maelekezo kuhusu utaratibu wa kuhakiki namba tambulishi, kutoa taarifa wanapopoteza au kuibiwa simu.


Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
18 December 2015


Popular Posts

Labels