Saturday, September 7, 2013

TWITTER YAIFUNGA TENA AKAUNTI YA AL SHABAAB


 

Akaunti ya Twitter ya kundi la wanamgambo wa Al Shabaab imesitishwa kwa mara nyingine.
Ujumbe kutoka kwa Twitter katika akaunti yake ya @HSMPress1 ulisema kuwa akaunti hiyo imefungwa, ingawa hapakuwa na maelezo kwa nini hatua hiyo ilichukuliwa.

Katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP kundi hilo lililaani hatua ya Twitter na kusema kuwa haitazaa matunda yoyote.

Mnamo siku ya Jumanne, Al Shabaab ilisema kuwa ilishambulia msafara wa magari ya rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, ambaye hakujeruhiwa.

Hata hivyo habari hizo zilipuuzwa na ofisi yake ikisema kuwa rais hakujeruhiwa kwani kifaa kililipuka mbali sana na msafara wake.

Baadaye kundi hilo lilituma ujumbe kwa Twitter uliosema kuwa ,''Mara nyingine hautaponea ''kwa mujibu wa ripoti za , AFP. Hata hivyo akaunti yake ya kiarabu ingali iko wazi.
 
Kwa mujibu wa sera ya Twitter, akaunti zinazotumika kutuma vitisho,zinapaswa kufungwa. Akaunti pia zinaweza kufungwa ikiwa zinatumiwa kwa shughuli zisizo halali.

Taarifa ya Al-Shabab ilisema kuwa haina akaunti nyingine ya Twitter kwa kiingereza na kuwaonya watumiaji wa mtandao huo kuwa wajiandae kwa akaunti zao kuvamiwa.

Akaunti ya Twitter ya kundi hilo kwa jina @HSMPress, ilisitishwa mwezi Januari baada ya kundi hilo kuitumia kutuma ujumbe wa kutisha kuwa lingewaua mateka wa Kenya na kisha kusema kuwa limefanya hivyo.

Wadadisi wamesema kuwa katika siku za nyuma, Marekani ililazimisha Twitter kufunga akaunti hiyo ingawa haikuwa na nguvu za kisheria kufanya hivyo.

Hata hivyo Twitter inasema kuwa hakuna kitu kinachoweza kuzuia Al Shabaab kuwa na akunti nyingine baada ya nyingine za kwanza kufungwa.

Al-Shabab ilifungua akauti yake mara ya kwanza mwezi Disemba mwaka 2011 baada ya wanajeshi wa Kenya , kwenda Somalia kupambana na wanamgambo hao.

Wanamgambo hao wamefurushwa Mogadishu pamoja na kutoka miji mingine ingawa bado wanadhibiti sehemu nyingi za Kusini mwa Somalia.
Chanzo:BBC Swahili.

 

Popular Posts

Labels